Hao hukithiri kusikiliza ili wapate kuzua, na hukithiri kula mali ya haramu ambayo hayana baraka yoyote, kama vile rushwa na riba na mengineyo. Basi wakikujia kukutaka uwahukumu, wewe wahukumu pindi ukiona hayo yana maslaha, au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao hawatokudhuru kwa lolote, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kukulinda na watu. Na ukihukumu baina yao basi hukumu kwa uadilifu alio kuamrisha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda waadilifu, naye huwahifadhi na huwalipa thawabu.
Ama ajabu ya watu hawa Mayahudi! Vipi wanataka hukumu yako na hali wao wanayo hukumu ya Mwenyezi Mungu imeandikwa katika Taurati? Na kinacho staajabisha ni kuwa wao huikataa hukumu yako inapo kuwa haikubaliani na mapendeleo yao, ijapo kuwa imewafikiana na ilivyo katika kitabu chao! Watu hawa sio miongoni mwa Waumini wanaoit'ii Haki.
Hakika Sisi tumemteremshia Musa Taurati. Ndani yake mna uwongofu unao endea Haki, na mna bayana yenye kutoa mwangaza unao nawirisha hukumu wanazo zihukumia Manabii, na wale walio safisha nafsi zao kwa ajili ya Mola wao Mlezi, na wanazuoni wenye kufwata njia ya Manabii, na wale walio chukua ahadi kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu kisibadilishwe, kwa kukilinda na kushuhudia kuwa hicho ndiyo Haki. Basi msiwakhofu watu mnapo hukumu, na nikhofuni Mimi tu, Mimi Mola wenu Mlezi, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Wala msizibadilishe Aya zangu nilizo ziteremsha kwa thamani duni ya kutaka starehe ya dunia, kama vile mrungura au kutaka cheo! Na wote wasio hukumu kwa mujibu alivyo teremsha Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa makafiri.
Tumewalizimisha Mayahudi katika Taurati wafuate sharia ya kisasi kwa ajili ya kuhifadhi maisha ya watu. Basi tukahukumu mwenye kuuwa auwawe. Mwenye kutofoa jicho la mtu atofolewe. Kadhaalika pua kwa pua, sikio kwa sikio, jino kwa jino, na jaraha hivyo hivyo lilipiziwe kisasi ikimkinika. (Hiyo ni hukumu ya Mayahudi kama ilivyo katika Kutoka 21.23-25; Mambo ya Walawi 24.18-21; Kumbukumbu la Torati 19.21. Katika Uislamu ipo fursa ya msamaha.) Mwenye kusamehe akatolea sadaka ile haki ya kulipiza kisasi kwa mkhalifu, basi hiyo sadaka huwa ni kafara kwake. Mwenyezi Mungu naye atamfutia sehemu ya madhambi yake. Na watu wasio hukumu kwa mujibu wa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wenye kudhulumu.