Na katika Siku hii ya leo utawadhihirikia uovu wa vitendo vyao, na itawazunguka adhabu ya yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhaara duniani.
Na mtu yakimpata madhara hutuomba kwa unyenyekevu; kisha tukimpa neema kwa kumfadhili, mtu huyo huyo husema: Sikupewa neema hizi mimi ila kwa ujuzi wangu nilio nao wa kujua kuchuma. Naye mtu huyu kasahau kuwa mambo si hivyo kama asemavyo, bali neema hizo alizo mneemesha Mwenyezi Mungu ni kama majaribio tu, ni mtihani, ili amdhihirishe nani mwenye kut'ii na nani mwenye kua'si. Lakini wengi wa watu hawatambui kama hayo ni majaribio na fitna.
Maneno kama haya waliyasema walio kuwa kabla ya washirikina hawa, na hayakuwalinda na adhabu hayo mali na starehe waliyo yachuma.
Yakawasibu makafiri walio tangulia malipo ya madhambi ya vitendo vyao, na madhaalimu miongoni mwa hawa wanao semezwa hivi sasa yatawapata vile vile malipo ya madhambi ya vitendo vyao. Wala hawa hawataiepuka adhabu.
Je! Hawa wanasema wayasemayo, wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humpa kwa kadiri atakacho kwa mujibu wa hikima yake? Hakika katika haya bila ya shaka ni mazingatio kwa watu wanao amini.
Ewe Muhammad! Sema kwa kufikisha kutokana na Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu walio jizidishia juu ya nafsi zao maasi, msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi yote. Hakika Yeye, peke yake, ndiye Mkuu katika kusamehe kwake na kurehemu kwake.
Enyi mlio jidhulumu nafsi zenu, rejeeni kwa Mwenye kuyamiliki mambo yenu yote, na Mlezi wenu. Na mfuateni Yeye kabla haijakujieni adhabu, tena hapo hapatakuwepo wa kukunusuruni na Mwenyezi Mungu na kukulindeni na adhabu yake.
Na fuateni yaliyo bora kabisa katika mliyo teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi, nayo ni Qur'ani Tukufu, kabla ya kukujieni adhabu kwa ghafla, na bila ya kujitayarisha, na hali nyinyi hamjui kuja kwake.
Rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na Msilimu kwake, na mfuate mafunzo yake, ili nafsi yenye dhambi isisema itapo iona adhabu: Ee msiba wangu kwa niliyo yawacha upande wa Mwenyezi Mungu na katika haki zake, na kwamba mimi nilikuwa duniani miongoni mwa walio kuwa wakiifanyia maskhara Dini yake.