Basi Qaruni hakusikia nasaha ya watu wake, na akasahau fadhila ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yake. Na akajifanya hajui kwamba Mwenyezi Mungu alikwisha waangamiza wengi walio mzidi yeye sana katika uwezo na mazoezi ya kuchuma mali kwa njia mbali mbali za uchumi. Na wakosefu hawaulizwi madhambi yao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua. Basi wataingizwa Motoni bila ya hisabu. Kuulizwa kwao ni kwa ajili ya kutahayarishwa tu.
Na Qaruni hakujali nasaha za watu wake. Akawatokea naye kajipamba mapambo yake. Wakadanganyika naye wale walio kuwa wanapenda starehe za maisha ya dunia, na wakatamani nao wangeli kuwa nayo mali na hadhi kubwa ya maisha kama aliyo pewa Qaruni
Ama wale ambao Mwenyezi Mungu amewaruzuku ilimu yenye manufaa hawakusalitika na hayo. Wakawaelekea walio danganyika kwa kuwanasihi wakiwaambia: Msiyatamani haya, wala msiiache Dini. Kwani yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ya thawabu na neema ni safi zaidi kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Na hiyo ni nasiha ya kweli ambayo hawaikubali ila wenye kuzipiga jihadi nafsi zao, na wakasubiri katika ut'iifu.
Mwenyezi Mungu akamdidimiza katika ardhi, na ardhi ikammeza yeye na nyumba yake na vyote vilio kuwemo ndani yake, mali na mapambo yake. Hakuwa na wasaidizi wa kumkinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na wala yeye mwenyewe hakuweza kujinusuru nafsi yake.
Na wale walio kuwa karibuni wakikitamani cheo chake cha duniani, wakawa wanatamka maneno ya masikitiko na majuto baada ya kuyafikiri yaliyo msibu yeye. Wakawa wanasema: Hakika Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake Waumini na wasio kuwa Waumini. Na humdhikisha amtakaye katika hao. Na wakawa wanasema kwa kushukuru: Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani kwa kutupa uwongofu tukafuata Imani, na akatuhifadhi tusiporonyoke angeli tutia katika mitihani kwa kutukubalia tuliyo kuwa tunayatamani, na akatufanyia kama alivyo mfanyia Qaruni. Hakika wanao ipinga neema ya Mwenyezi Mungu hawafanikiwi kwa kuokoka na adhabu yake.
Hayo ndio makaazi ambayo umesikia khabari zake, ewe Mtume, na zikakufikia sifa zake, nayo ni Pepo. Tumeiweka makhsusi kwa ajili ya Waumini wat'iifu, wasio taka kujipa ubora na utukufu wa kidunia, na wala hawapotoki kuendea ufisadi na maasi. Na mwisho mwema ni wa wale ambao nyoyo zao zimejaa khofu ya Mwenyezi Mungu, na wanatenda yanayo mridhisha Yeye.
Mwenye kuja na wema, nao ni Imani na vitendo vyema, atapata malipo marudufu kwa ajili yake. Na mwenye kuja na uovu, nao ni ukafiri na maasi, halipwi ila mfano wa vitendo vyake viovu.