Baada ya kwisha ondoka wale watu, Ibrahim aliwaendea masanamu akayavunja vipande vipande, isipokuwa sanamu kumbwa, hilo aliliacha ili wapate kuliregea waliulize yalio wasibu miungu yao nalo halikujibu kitu, kwa hivyo upotovu wa ibada yao ikabainika.
Baada ya kwisha ona yaliyo wapata miungu yao wakasema: Nani aliye itendea haya miungu yetu? Hakika mtu huyu hapana shaka ni katika walio jidhulumu wenyewe kwa adhabu itayo mpata..
Kuwanabihisha upotovu wao, alisema kwa kuwakejeli: Hili kubwa lao ndilo lililo tenda hayo! Iulizeni hiyo miungu aliyo yatenda huyu, kama kweli inaweza kujibu suala yenu!
Wakazirejea nafsi zao wakiifikiria ile ibada yao kuabudu vitu visivyo mnufaisha yeyote wala haviwezi kujitetea wenyewe. Wakayaona makosa yao. Baadhi yao wakasema: Ibrahim si katika walio dhulumu, bali nyinyi ndio madhaalimu kwa kuabudu vitu visio stahiki kuabudiwa.
Kisha wakarejea tena, wakaacha uwongofu, wakarudia upotovu. Wakamwambia Ibrahim: Hakika wewe umekwisha jua kuwa haya masanamu tunayo yaabudu hayasemi kitu. Basi vipi unatutaka tuyaulize?
Ibrahim akasema: Ikiwa hali yao haya masanamu ni hii, hayawezi kitu, na nyinyi ndio makhusiano yenu nao ni hivi, basi nyinyi mmekuwa mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, na badala yake mnaabudu vitu visivyo kupeni faida hata chembe mkiviabudu, wala havikudhuruni kwa lolote mkiviachilia mbali?
Aibu yenu! Nyinyi na miungu yenu mmelaanika! Mnaacha fikra zenu zipotee, na mnapuuza kuzingatia? Bila ya shaka haya masanamu hayafai kuabudiwa!
Wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Mchomeni moto mpate kuinusuru miungu yenu kwa mateso haya, ikiwa nyinyi mnataka kufanya kitu cha kuiunusuru miungu yenu.
Na tukamwokoa yeye na Luut'i na njama zilizo pangwa, wakaelekea kwenye nchi tuliyo ijaalia kheri nyingi kwa watu wote, na tukawapeleka huko Manabii wengi.
Na tukampa Ibrahim mtoto Is-haq, na kutokana na Is-haq tukampa Yaaqubu, zaidi kuliko aliyo taka. Na wote wawili, Is-haq na Yaaqubu tuliwajaalia kuwa ni watu wema.