Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kushukuriwa kwa wema, anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye amemteremshia mja wake, Muhammad, hii Qur'ani. Na wala hakujaalia kuwa ndani yake kipo chochote cha dosari, kilicho kwenda kombo na kuacha usawa. Bali ndani yake mna Haki tupu, isiyo na shaka yoyote.
Na Mwenyezi Mungu ameijaalia Qur'ani imesimama, imenyooka sawa sawa katika mafunzo yake ili kuwaonya wanao kufuru na kukataa, kuwa watapata adhabu kali itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na iwape bishara njema wanao isadiki, ambao wanatenda vitendo vyema, ya kwamba watapata malipo mazuri.