Walipo kuja wachawi kwa Firauni walimwambia: Je! Tutapata kwako ujira mkubwa pindi tukishinda?
Wakazitupa kamba zao na fimbo zao, na watu wakazugwa wakaona kama ni nyoka wanakwenda. Wakaapa kwa utukufu wa Firauni na nguvu zake hapana shaka hawa leo watashinda
Musa tena akatupa fimbo yake. Mara ikawa joka kubwa likaingia kuvimeza vile walivyo vizua kwa uchawi, navyo ni kamba na fimbo, wakidanganya kuwa ni nyoka wanao kwenda.
Firauni kwa kukasarika kuwa wale wachawi wamemuamini Musa bila ya yeye kuwapa ruhusa, aliwatishia ya kwamba yeye ndiye mwalimu wao aliye wafunza fani za uchawi, na watakuja jua adhabu itakayo wateremkia. Akawaambia: Nitakata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata wa kulia huu kwa wa kushoto huu, na kinyume cha hayo. Na nyote nitakutundikeni juu ya misalaba.
Wachawi wakasema: Hapana la kutudhuru sisi kwa adhabu unazo tutishia, kwani sisi ni wenye kurejea kwenye malipo ya Mola wetu Mlezi. Na Yeye ndiye mbora wa kulipa na mbora wa kuadhibu.
Hakika sisi tunataraji Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu tuliyo yafanya zamani, kwa kuwa sisi ndio wa mwanzo wa Waumini katika kaumu yako.
Na Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Musa a.s. atoke usiku usiku pamoja na Waumini miongoni mwa Wana wa Israili, ilipo kuwa tena haiwi kumsubirisha Musa. Mpango ukawa wa makundi mawili kwamba atangulie Musa na kaumu yake, na Firauni afuatie na kaumu yake, mpaka waingie katika maingilio ya njia ya baharini, na Mwenyezi Mungu awateketeze.
Firauni akawatuma askari wake katika miji ya mamlaka yake, wawakusanye wenye maguvu katika kaumu yake, alipo jua kuwa Musa kesha toka na Wana wa Israili, ili awazuie lile walilo kusudia.
Tukawatoa Firauni na askari wake kwenye nchi yao iliyo fanana na mabustani yapitiwayo na mito kati yao, wakaangamia kwa kujitenga kwao na Haki, na kuchochewa kutaka kumfuatia Musa, kama ilivyo kuja katika Aya tatu zilizo tangulia.
Ni kutoka kama huku kwa ajabu tulivyo kueleza ndivyo tulivyo watoa, na tukawapa ufalme huo na kila namna ya neema zilizo kuwamo Wana wa Israili, baada ya kuwa masikini hawana mbele wala nyuma.