Na tukawafanya mashetani wamtumikie kwa kuzamia chini baharini kumletea lulu na marijani; na wakifanya kazi nyenginezo, kama kujenga ngome na majumba ya kifalme. Na Sisi tulikuwa tukiwaangalia katika kazi zao hizo, basi hapana hata mmoja wao aliye pata shida, wala hawakuvunja amri ya Suleiman.
Ewe Nabii! Mtaje Ayyubu, pale alipo mwita Mola wake Mlezi, na maradhi yalikwisha mdhoofisha, na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika nimesibiwa na madhara na yananiuma! Na Wewe ni Mbora wa wanao rehemu..
Tukamwitikia kwa aliyo yaomba, tukamwondolea madhara, na tukampa watoto kwa kadri ya waliyo kwisha kufa. Na tukamwongezea mfano wa wale, kuwa ni rehema iliyo tokana na fadhila yetu, na pia ni kuwa ni kumbusho kwa wenginewe wanao tuabudu ili wapate nao kusubiri kama alivyo subiri yeye, na watumai kupata rehema ya Mwenyezi Mungu kama alivyo tumai yeye.
Ewe Nabii! Taja kisa cha Yunus, aliye mezwa na samaki..Pale alipoona dhiki kwa vile watu wake walipo puuza wito wake, naye akawahama akenda mbali nao na huku amewakasirikia. Akadhani ya kuwa Mwenyezi Mungu amemruhusu kuwahama, na kwamba haitopita hukumu juu yake. Samaki akammeza, na akaishi katika kiza cha bahari. Akamwita Mola wake Mlezi kwa kumnyenyekea, na kuungama aliyo kuwa nayo, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Wewe. Ninakutakasa na kila lisio kuelekea Wewe. Ninaungama kuwa hakika mimi nilikuwa miongoni mwa walio dhulumu nafsi zao kwa kutenda yasio kupendeza.
Tukamwitikia kwa aliyo kuwa akiyaomba, na tukamvua na dhiki aliyo kuwa nayo. Na mfano wa hivi ndivyo tunavyo waokoa Waumini wanao ungama makosa yao, na wakatuomba kwa usafi wa moyo.
Na kitaje kisa cha Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi baada ya kwisha ona uweza wake Subhanahu kwa alivyo mtia katika nafsi yake matarajio ya rehema yake. Alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Usiniache mpweke bila ya kuwa na mrithi, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. Kwani Wewe ndiye utakaye baki baada ya kumalizika viumbe vyote.
Tukamtimizia matumaini yake, na tukamwitikia dua yake, na tukamtunukia juu ya ukongwe mwanawe, Yahya, tukamfanya mkewe tasa aweze kuzaa. Hakika wasafi hao Manabii walikuwa wepesi wa kutenda kheri tunayo waitaka waitende, na wanatuomba kwa kutumai rehema yetu, na kuikhofu adhabu yetu. Na walikuwa hawamtukuzi mtu wala hawamwogopi mtu isipo kuwa Sisi tu.