Ewe Nabii! Sema: Sikuhadharisheni kwa maneno yanayo tokana nami. Lakini nakuhadharisheni kwa Wahyi (Ufunuo) unao tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu ulio nijia mimi. Na huo ni wa Haki na kweli. Lakini hao kwa sababu ya kupuuza kwao kurefu kuipuuza Sauti ya Haki, Mwenyezi Mungu ameyaziba masikio yao mpaka wakawa kama viziwi. Na kiziwi hasikii Wito anapo hadharishwa na adhabu!
Na kuwa na yakini kuwa nao wakisibiwa hata na chembe ya adhabu ndogo wanayo ifanyia maskhara, hupiga kelele kwa khofu wakisema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa tunajidhulumu nafsi zetu, na tukiwadhulumu wenginewe, tulipo yakataa tuliyo ambiwa.
Na Sisi tunaweka mizani ya kupimiwa kwa uadilifu Siku ya Kiyama. Basi hadhulumiwi mtu kwa kupunguziwa wema wake au kuongezewa maovu yake. Hata ikiwa ni kiasi ya uzani wa chembe ndogo hii tutaileta na tutaihisabu. Na yatosha kuwa ni Sisi ndio wa kuhisabu. Basi hapana atakaye dhulumiwa kitu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 47: "Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.": Aya hii tukufu inaonyesha kuwa chembe ya khardali ni hadi ya udogo katika mizani. Imethibitika kwa majaribio ya sayansi kuwa Kilogram ya chembe za khardali ni chembe 913,000. Kwa hivyo chembe moja ya khardali ni takriban sehemu moja katika elfu ya gram, yaani ni takriban sawa na Miligram moja. Na huu ni uzito mdogo kabisa unao juulikana katika mbegu za mimea mpaka sasa. Kwa hivyo hutumiwa katika kupimiwa vitu vidogo vidogo kabisa.
Na Musa na Haaruni tuliwapa Taurati ya kupambanua baina ya kweli na uwongo, na halali na haramu. Na juu ya hivyo hiyo ni nuru ya kuwaongoa watu wafuate njia ya kheri na uwongozi mwema, na ni kumbusho la kuwafaa wachamngu...
Ambao wanamkhofu Muumba wao Mwenye kumiliki mambo yao yote, juu ya kuwa wako mbali na watu, na wala hawamwoni mtu. Nao wamo katika khofu ya daima kuikhofu Siku ya Kiyama.
Na hii Qur'ani ni kumbusho, lenye kheri nyingi. Tumekuteremshieni kama tulivyo mteremshia Musa. Basi yawaje nyinyi muikatae, na hali nyinyi ndio mnao stahiki zaidi kuiamini kuliko watu wote!
Na hakika Sisi tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu na fikra ya kutafuta Haki kwa usafi wa niya kabla ya Musa na Haaruni. Na Sisi ni Wenye kujua vyema hali yake na fadhila zake zilizo mfanya astahiki kuchukua Utume.
Ewe Nabii! Kumbuka pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na watu wake kuwaonya juu ya masanamu waliyo kuwa wakishughulikia kuyaabudu: Ni nini haya masanamu ambayo nyinyi mmeshika kuyaabudu?
Wakasema: Je! Umetujia kwa haya uyasemayo na hakika ya kweli unayo iamini, au kwa maneno haya wewe ni katika wanao fanya pumbao na mchezo tu bila ya kuwa na maana yoyote?
Akasema: Hapana maskhara katika niyasemayo. Bali Mola wenu Mlezi anaye stahiki peke yake kutukuzwa na kuogopwa na kuabudiwa ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akazileta bila ya kuwapo mfano wake wa kuigiza. Basi ni haki yake Yeye tu peke yake kuabudiwa. Na mimi kwa haya niyasemayo ni katika wenye hakika ambao hunena wanayo yashuhudia na wanayajua.
Na akasema moyoni mwake: Naapa kwa Mwenyezi Mungu, nitayafanyia vitimbi haya masanamu yenu niyavunje pale mtapo ondoka, ili mpate kuona upotovu wenu.