Akaja Firauni, na mataifa mengine yaliyo kufuru kabla yake, na wale jamaa walio acha mwendo wa haki na vitendo vya maumbile wakafanya vitendo vichafu kabisa hata miji yao ikapinduliwa juu chini.
Kila umma katika hawa walimuasi Mtume wa Mola wao Mlezi. Naye Mwenyezi Mungu akawashika kwa kuwaadhibu kwa mshiko ulio zidi ukali.
Maji yalipo zidi ukomo wake, na yakapanda juu ya milima katika tukio la tofani ya Nuhu, Sisi tulikupandisheni, yaani kwa kuwapandisha wazee wenu wa asli, katika safina inayo kwenda baharini.
Ili kulifanya tukio hilo la kuwaokoa Waumini na kuwazamisha makafiri liwe zingatio na mawaidha kwenu, na lihifadhiwe na kila sikio lenye kuhifadhi linalo sikia.
Na Malaika pembezoni mwake, na wapo Malaika wanane siku hiyo watakao beba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi, juu ya Malaika hawa wengine.
Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema akiwatangazia furaha yake walio karibu naye: Chukueni msome kitabu changu!
Kuleni na mnywe kwa kula na kunywa kusio na karaha, wala maudhi, kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo kwisha vitanguliza katika siku za duniani zilizo pita.
Ama mwenye kupewa kitabu chake kwa mkono wake wa kushoto atasema kwa majuto na huzuni: Laiti kuwa sikupewa kitabu changu,