Na wewe si chochote ila ni mmoja wetu sawa na sisi kwa utu. Basi vipi ujipe ubora kuliko sisi kwa Utume? Nasi tunaamini kuwa wewe ni mwongo wa kubobea.
Basi hebu tuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni ikiwa ni katika wasemao kweli kwa huu ujumbe wako! Na chini ya shauri hii kwa hakika pana kila namna ya ubishi.
Shuaibu akasema: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi, upeo wa kujua, wa maasi yote myatendayo, na adhabu mnayo stahiki. Yeye atakuteremshieni hayo kwa wakati wake alio ukadiria. Na huu ndio hadi ya mwisho wa kumwachilia Mwenyezi Mungu kila kitu, na kuwatisha hao makafiri.
Lakini wao waliendelea kumkadhibisha. Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa adhabu ya joto kuu mno. Wakawa wanatapa tapa hawana pa kukimbilia. Walipo pata kiwingu cha kuwapa kivuli kukinga mwako wa jua walijikusanya chini yake. Mwenyezi Mungu akawateremshia moto, ukawateketeza wote katika siku ya kitisho kikubwa mno.
Hakika adhabu iliyo wateremkia watu wa Machakani kuwa ni malipo ya uasi wao, ni dalili ya ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na hawakuwa wengi wa watu wako wenye kusadiki.
Na hakika hii Qur'ani iliyo tajwa ndani yake visa vya kweli imeteremshwa kutoka kwa Mwenye kuumba walimwengu wote, Mwenye kumiliki mambo yao, na Mlezi wao. Basi khabari zake ni za kweli. Na hukumu yake inatimizwa mpaka Siku ya Kiyama.
Je! Hawa wenye inda wanaikataa Qur'ani na hali wao wanayo hoja inayo onyesha ukweli wa Muhammad s.a.w., nayo ni ilimu ya wanazuoni wa Wana wa Issraili juu ya Qur'ani kama ilivyo katika vitabu vyao?
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watu wa Makka wameghurika na kuchelewesha kwangu kuwaadhibu, basi ndio wanaihimiza? Anakusudia Subhanahu Aliye takasika kuzisafihi akili zao kwa sababu ya kuhimiza kwao adhabu juu ya kuwaonya na kuwatisha.