Basi wakaendelea kushikilia kumkanusha. Mwenyezi Mungu akawafanyia haraka kuwateketeza. Hakika katika hayo aliyo wateremshia Mwenyezi Mungu kina A'di kwa kuwa ni malipo kwa ukanushi wao, ni hoja inayo juulisha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na si wengi katika wanao somewa khabari za A'adi walio Waumini.
Wala sitaki kwenu ujira wowote kwa hii nasaha yangu na uwongozi wangu. Ujira wangu uko kwa Mwenye kumiliki walimwengu wote.
Wewe si chochote ila ni mmoja unaye fanana na sisi kwa ubinaadamu, basi yawaje uwe bora kuliko sisi kwa Unabii na Utume? Na ukiwa wewe ni mkweli katika madai yako basi lete muujiza wa kuonyesha uthibitisho wa Utume wako.
Saleh akawaambia - alipo pewa na Mwenyezi Mungu ngamia jike kuwa ni muujiza wake: Huyu hapa ngamia jike wa Mwenyezi Mungu, amekutoleeni kuwa ni Ishara. Yeye ana sehemu yake ya maji katika siku moja; siku hiyo msinywe nyinyi. Na nyinyi mna sehemu yenu siku nyengine. Kunyweni siku hiyo.
Basi ikawateketeza adhabu aliyo waahidi Swaleh, wala majuto hayakuwakinga na adhabu ya ukosefu wao. Hakika katika kusimulia kisa chao pana dalili ya kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kuwateketeza makafiri na kuwaokoa Waumini. Na si wengi katika watu wako wenye kuamini.