Na Sisi tumeweka mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
Na yeyote katika hao mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo onekana wazi.
Na tumekuumbieni ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
Na tumekujaalieni katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
Na hapana chochote cha kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu, kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
Na Sisi tulipeleka pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani "Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides" na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko. Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
Na kila mmoja wenu ana muda wake alio pimiwa. Sisi ndio tunao ujua. Tunawajua walio tangulia kwa kufa na kuwa hai, na pia wanao taakhari.
Na hakika walio tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake. Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
Na Sisi katika kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
Ewe Nabii! Kumbuka asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote, kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
Nikisha kamilisha kumuumba, na nikampulizia roho ambayo ninaimiliki, basi teremkeni kwa nyuso zenu mkimsujudia, kwa kumwamkia na kumhishimu.