Wala sidai kuwa nafsi yangu haitelezi; kwani ni tabia ya nafsi kumili kwenye matamanio, na kupendelea maovu na shari. Isipo kuwa nafsi aliyo ilinda Mwenyezi Mungu na akaiweka mbali na maovu. Na hakika mimi ninatumai rehema ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake, kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe dhambi za wenye kutubu, na yu karibu wa kuwarehemu waja wake walio kosa.
Usafi wa Yusuf ulipo dhihiri kwa mfalme, aliazimu amwite. Akawatuma watu wake wamlete awe wake yeye mwenyewe wa kumsafia niya. Basi alipo hudhuria na yakapita baina yao mazungumzo, mfalme akaathirika na utukufu wa Yusuf kwa usafi wa nafsi yake, na ubora wa rai zake! Akamwambia: Sasa wewe kwangu utakuwa na cheo cha hishima kilicho thibiti. Na wewe ni muaminifu kwangu ninaye kuamini.
Mfalme akajua kwake Yusuf kuwa yeye ni muangalizi mwema na mweza wa kazi yake. Na Yusuf akahisi hayo. Hapo akataka amfanye waziri akamwambia: Nitawalishe juu ya khazina zote za mamlaka yako, na ghala za nchi yako. Kwani mimi kama ulivyo yakinika mwenyewe naweza kuendesha mambo ya serikali, nami ni mlinzi, na najua kupanga na kuendesha mambo.
Mfalme alilikubali ombi lake, akamfanya waziri wake. Hivyo basi Mwenyezi Mungu alimneemesha Yusuf kwa neema nzuri, akampa madaraka na uwezo katika nchi ya Misri, akienda humo atakapo. Na hii ndiyo shani yake Mwenyezi Mungu kwa waja wake, humpa neema yake amtakaye katika wao, wala hawanyimi thawabu zao, bali huwapa ujira wao wa wema wautendao kwa kuwalipa mema hapa hapa duniani.
Na malipo yao ya Akhera ni bora zaidi na yanalingana zaidi na hao wanao msadiki Yeye na Mitume wake, na ikawa wanaingojea Siku ya Hisabu na wanaikhofu.
Ukame ukazidi kushtadi katika nchi jirani na Misri. Ikawapata watu wa Yaa'qub shida vile vile kama ilivyo wapata wengineo. Watu walikwenda Misri kutoka kila pande baada ya kujua matengenezo ya Yusuf ya kuweka akiba chakula, na kujitayarisha kwake kwa miaka ya ukame. Yaa'qub aliwatuma wanawe wende kutafuta chakula, lakini akabaki naye nduguye Yusuf kwa mama kwa kumkhofia. Wale watoto wake walipo fika Misri wakenda moja kwa moja kwa Yusuf, naye akawatambua, lakini wao hawakumjua.
Yusuf akaamrisha wakaribishwe ugeni, na wapewe mahitaji wanayo yataka. Wakapewa hayo. Akaingia kuzungumza nao na kuwauliza hali zao kama mtu asiye wajua! Naye anawajua vyema. Nao wakamwambia kuwa wamemwacha ndugu yao mmoja kwa baba yao, kwani hapendi kuachana naye. Naye huyo ni Bin-yamini nduguye Yusuf kwa baba na mama. Basi yeye akasema: Mwacheni ndugu yenu aje nanyi, wala msiogope chochote. Nyinyi mmekwisha ona vipi ninavyo kutimizieni vipimo vyenu, na ninavyo kukirimuni.
Nduguze wakasema: Tutajaribu kusema na baba yake ageuze rai yake, iondoke khofu yake juu ya mwanawe. Na sisi tunakuhakikishia kuwa hatutokasiri wala kulegalega katika hayo.
Walipo taka kuondoka aliwaambia wafwasi wake: Watilieni thamani ya bidhaa yao waliyo kuja nayo humo humo pamoja na mizigo yao, ili waione watakapo rudi kwa watu wao, wapate kurejea tena kwa kutumai kupewa chakula kwa kuamini kuwa tunatimiza ahadi, na wawe na imani ya usalama wa ndugu yao, na baba yao azidi kutua nafsi yake.
Walipo rejea kwa baba yao walimsimulia kisa chao na Mheshimiwa wa Misri, na upole wake kwao, na kwamba amewaonya kuwa atawanyima kuwapimia chakula baadae ikiwa hatokuwa nao Bin-yamini; na kwamba amewaahidi kuwatimizia kipimo na atawatukuza pindi wakirudi na ndugu yao. Wakamwambia baba yao: Mwache ende nasi ndugu yetu, kwani ukimpeleka yeye tutapimiwa chakula cha kutosha tunacho kihitajia. Nasi tunakuahidi ahadi ya nguvu ya kwamba tutafanya juhudi kumlinda.