Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo korogeka ovyo, na wasiwasi wa kuzuka tu katika nafsi ya mtu! Na sisi si wenye kujua tafsiri ya ndoto za ovyo ovyo.
Akasema yule mtu aliye okoka katika wawili alio kuwa nao Yusuf gerezani, na akakumbuka wasia wa Yusuf, baada ya kupita muda mrefu: Mimi nitakwambieni tafsiri ya ndoto aliyo itaja mfalme. Nipelekeni kwa huyo mwenye ilimu ya kuifasiri.
Yule mtumishi wa kumletea mfalme ulevi akenda kwa Yusuf, akamwita: Yusuf! Ewe uipendaye kweli! Tueleze nini maana ya ndoto ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na ndoto ya mashuke saba mabichi na mengine makavu? Nataraji kurejea kwa watu nami nina fatwa yako, ili nao wapate kujua maana yake, na waujue ujuzi wako na fadhila yako.
Yusuf akasema: Tafsiri ya ndoto hizo ni kuwa mtalima katika ardhi ngano, na shairi kwa muda wa miaka saba mfululizo kwa ukulima wa juhudi. Mtacho vuna kihifadhini, mkiache katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtacho kila katika miaka hiyo, kwa uangalizi mzuri. Aya hii inawafikiana na ilimu za kisasa kuwa kuweka punje katika mashuke yake inakuwa ni hifadhi zisiharibike kwa hali ya hewa na mengineyo, na juu ya hivyo faida yake ya chakula inabaki kwa ukamilifu zaidi.
Kisha baada ya miaka hii ya neema itakuja saba ya ukame. Mtakula kile mlicho weka akiba, isipo kuwa kidogo mtacho kificha na kukihifadhi, ili kiwe mbegu ya kupandia baadae
Kisha baada ya miaka hiyo ya ukame utakuja mwaka watu watasaidiwa kwa mvua, na watakamua zabibu na zaituni, na kila cha kukamuliwa.
Mfalme akamwona Yusuf atakuwa na faida naye kwa ule uwezo wake kuifasiri ndoto yake, na akaazimia amwite. Akawaamrisha wasaidizi wake wamlete. Alipo mfikia mjumbe akamwabia kuwa mfalme anamtaka, khabari hiyo haikumpapatisha, juu ya kuwa ina bishara ya kufunguliwa kwake. Wala kule kutamani kutoka kwa mfungwa kwenye dhiki za jela na taabu zake hakukuitikisa subira yake. Akakhiari angoje mpaka idhihirike kuwa hana makosa kuliko kufanya haraka kutoka na huku yale aliyo tuhumiwa bado yamemganda. Akamwambia mjumbe: Rejea kwa bwana wako umtake ayaangalie tena yale mashtaka niliyo shitakiwa, awaulize wale wanawake walio kusanywa na mke wa Mheshimiwa kwa kunifanyia hila mimi, wakababaika na wakajikata mikono yao: Je! Walipo toka kwenye yale majaribio walikuwa wanaamini kuwa mimi sina makosa na safi, au waliniona ni mchafu na mzinifu? Mimi nataka haya ipate kuonekana hakika katika macho ya watu. Ama Mola wangu Mlezi anavijua vyema vitimbi vyao!
Mfalme akawakusanya wale wanawake, na akawauliza: Ilikuwa vipi hali yenu pale mlipo jaribu kumkhadaa Yusuf aghafilike na wema wake na usafi wa nafsi yake? Je, mlimwona amemili kwenu? Wakamjibu: Mwenyezi Mungu ametakasika! Hakumsahau mja wake hata uchafuke usafi wake. Sisi hatukuona kwake lolote la kumtia dosari. Hapo basi wema ukapata nguvu katika moyo wa Zuleikha (mke wa Mheshimiwa) akaingia kusema: Sasa kweli imedhihiri! Ni mimi ndiye niliye mkhadaa, na nikajaribu kumzaini kinyume na nafsi yake kwa kumghuri. Lakini yeye alishikilia usafi wake! Na sasa nahakikisha kuwa yeye ni katika watu wa kweli. Na ni haki tupu alipo nirudishia tuhuma mimi na kunitia makosani!
Haya mimi naungama kwa kweli ninayo itoa, apate kuwa na yakini Yusuf kuwa mimi sikuchukua fursa ya kuto kuwepo alipo kuwa gerezani nikaendelea na khiyana, na nikamdhulumu kwa kumtuhumu. Na kwa kuwa hakika Mwenyezi Mungu haijaalii kufanikiwa mipango ya makhaini.