Na tuliwaweka vyema Wana wa Israili wakaishi katika nchi nzuri na huku wakiihifadhi Dini yao, nao wako mbali na dhulma iliyo kuwa ikiwapata; riziki na neema zimewajalia. Lakini mara baada ya kuonja neema ya utukufu baada ya unyonge, yaliwasibu maradhi ya kufarikiana. Wakakhitalifiana juu ya kuwa imekwisha bainika kweli na uwongo! Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama, na atamlipa kila mmoja kwa alilo tenda.