Ewe Mtume! Umeangalia, ukamwona huyo mwenye kufanya matamanio yake ndiye mungu wake wa kumuabudu, akamnyenyekea, na akamt'ii, na akaiacha Njia ya Haki na hali anaijua, na akaziba masikio yake asisikie waadhi, na moyo wake asiamini Haki, na akabandika vitanga vya macho asione ya kuzingatiwa? Basi nani wa kumwongoa mtu huyu baada ya kwisha puuzwa na Mwenyezi Mungu? Je! Mnaacha kutazama ili msipate kukumbuka?
Na walisema wenye kukanya kufufuliwa: Hapana uhai ila huu uhai wa duniani tu tulio nao sasa. Tunaishi na tunakufa. Na hapana nyuma ya hayo uhai baada ya kwisha kufa. Na hapana cha kututeketeza isipo kuwa kupita dahari, yaani zama na wakati. Wala wao hawasemi hayo kwa ujuzi na kuwa na yakini, bali ni kwa kudhania na kukisia tu.
Na ukiwasomea Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi zenye kuonyesha uwezo wake wa kufufua, huwa hawana hoja ila kusema - kwa kuikimbia haki : Wafufueni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika kudai kuwa kupo kufufuliwa.
Ewe Muhammad! Waambie: Mwenyezi Mungu amekupeni uhai duniani nanyi hamkuwa chochote, kisha anakufisheni unapo timia wakati wenu. Kisha atakukusanyeni Siku ya Kiyama, na hapana shaka ya kukusanywa huko. Lakini wengi wa watu hawaujui uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa sababu ya mapuuza yao kuzingatia dalili ziliopo. Na huyo Muweza wa hayo pia ni Muweza wa kuwaleta baba zenu.
Na ni wa Mwenyezi Mungu pekee ufalme wa mbingu na ardhi, kwa kuumba, kumiliki, na kupanga. Na itapo fika Saa ya Kiyama, siku hiyo watakhasiri wenye kufuata upotovu.
Ewe unaye semezwa! Utawaona siku itapo fika Saa watu wa kila dini wamekalia magoti kwa khofu waliyo nayo kungojea kuitikia wito. Kila umma utaitwa kwenye daftari la vitendo vyao, na wataambiwa: Leo mtalipwa sawa malipo ya mliyo kuwa mkiyatenda duniani.
Na wataambiwa: Hichi hapa kitabu chetu tulimo sajili vitendo vyenu, nanyi mmekichukua kwa mikono yenu, kinataja juu yenu yale mliyo yatenda kwa ushahidi wa kweli. Hakika Sisi tulikuwa tukiwataka Malaika waandike, ili tupate kukuhasibieni yaliyo tokana nanyi.
Basi ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia katika Pepo yake. Malipo hayo ndio kufuzu kulio bainika, kulio wazi.
Na ama walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake wataambiwa kwa kuwahizi: Kwani hawakukujilieni Mitume wangu? Hamkusomewa Aya zangu, nanyi mkajiona bora hamfai kuikubali haki, na mkawa kaumu ya makafiri?
Enyi mnao kanya kufufuliwa! Akikwambieni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba agano la Mwenyezi Mungu la kuwalipa ni haki yenye kuthibiti, na Saa haina shaka itakuja, nyinyi mkisema: Sisi hatujui chochote khabari ya hiyo Saa ya Kiyama, wala ukweli wake; na sisi ni dhana ya kudhania tu kuwa hiyo Saa itakuja, wala hatuna yakini kuwa itatokea.