Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye anzisha uumbaji tangu mwanzo, na kisha baada ya kupotea kwake akaurejesha kama ulivyo kuwa? Na nani anaye kuteremshieni riziki kutoka mbinguni, na akaitoa kwenye ardhi? Hakuna mungu pamoja na Mwenyezi Mungu atendaye hayo. Sema, ewe Mtume, kuwatahayarisha na kuwakanya: Kama nyinyi mnaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi tupeni hoja ya hayo, ikiwa mnadai kuwa nyinyi ni wasema kweli. Na wala hayataweza kuwa hayo kwenu.
Sema, ewe Mtume: Hakika mwenye kutenda yote haya peke yake ndiye Yeye Subhanahu aliye tengeka peke yake kwa kuyajua mambo ya ghaibu yalioko mbinguni na duniani. Na Yeye huyo ndiye Mwenyezi Mungu wa pekee. Wala watu hawajui wakati gani watafufuliwa kutoka makaburini kwao kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa.
Ujuzi wao wa Akhera umefuatana na ujinga, na huo ukawapelekea kuitilia shaka. Nao wamekuwa vipofu hawaitambui Haki katika jambo lolote, kwa sababu upotovu umefisidi fahamu zao.
Wakasema makafiri kwa kukanya kufufuliwa: Hivyo sisi tukisha kuwa mchanga, na ikisha oza miili yetu na ya baba zetu walio tutangulia, ndio tutarejeshwa tutolewe upya tuwe wahai?
Muhammad ametuahidi kuwa tutafufuliwa, kama Mitume walio tangulia walivyo waahidi baba zetu. Ingeli kuwa hayo ni kweli, basi yangeli kwisha kuwa. Haya si chochote ila ni uwongo tu wa watu wa kale.
Ewe Mtume! Waambie: Tembeeni duniani, na mtazame mabaki ya yaliyo wapata walio kadhibisha, nayo ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Huenda labda mkayazingatia haya, na mkaikhofu adhabu ya Akhera.
Ewe Mtume! Usiwahuzunukie makafiri wasio kufuata. Kwani kwa hakika waajibu wako ni kufikisha Ujumbe tu. Wala usiwe na dhiki kifuani mwako kwa sababu ya hila zao na vitimbi vyao. Kwani hakika Mwenyezi Mungu atakupa ushindi juu yao.
Na makafiri wanafanya ukomo wa juhudi yao kukanusha, na wanaihimiza adhabu kwa kusema: Lini, basi, itakuwa hiyo adhabu ambayo mnatutishia kuwa itakuja, ikiwa nyinyi mnasema kweli kuwa adhabu itawashukia wanao kanusha?
Na hakika Mwenyezi Mungu Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ni Mwenye neema na hisani kwa watu wote. Na katika rehema zake ni kuakhirisha hiyo adhabu kwa hao wanao kadhibisha. Lakini watu wengi hawaelewi fadhila za Mwenyezi Mungu wala hawamshukuru.
Ewe Mtume! Hakika Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi, hapana shaka anajua kila wanalo lificha na wanalo litangaza, ikiwa maneno au vitendo viovu. Naye atakuja walipa kwayo.
Na hapana kilicho fichikana cha ghaibu, na kiwe kidogo vipi au duni, mbinguni au katika ardhi ila Mwenyezi Mungu anakijua, na amekidhibiti katika Kitabu cha Haki kilioko kwake.
Hakika Kitabu hiki alicho teremshiwa Muhammad kinawawekea wazi Wana wa Israili ukweli wa yaliyo kuja katika Taurati, katika mambo ya itikadi na hukumu na hadithi. Na kinawarudisha kwenye kweli katika mambo waliyo khitalifiana kwayo.