Na waulize Mayahudi, kwa kuyachukia walio yafanya wenzao walio watangulia, khabari ya kijiji, nacho ni Elat, kilicho kuwa karibu na bahari. Wakaazi wake walivunja amri ya Mwenyezi Mungu ya kupiga marfuku kuvua samaki siku ya Jumaamosi, kuwa hiyo ni siku ya ibada tu kwao. Na siku hiyo samaki walikuwa wakiwajia vururu juu ya maji. Na siku isiyo kuwa Jumaamosi samaki walikuwa hawaji. Huo ni mtihani wa Mwenyezi Mungu! Na kwa mfano wa mtihani huo, au majaribio hayo yaliyo tajwa, ndio tunawajaribu kwa majaribio mengine kwa sababu ya upotovu wao unao endelea, ili adhihiri mwema na mbaya.