Mwenyezi Mungu amezitaja neema zake juu ya kaumu ya Musa. Akafahamisha kuwa aliwafanya makundi thinaashara, (kumi na mbili) na akawafanya mataifa, na kila taifa likawa na mpango wao, ili kuzuia uhasidi na kukhitalifiana. Na walipo taka watu wake maji jangwani, alimfunulia Musa alipige jiwe kwa fimbo yake. Akalipiga, zikatibuka kutoka kwenye hilo jiwe chemchem kumi na mbili kwa idadi ya kabila zao. Kila kabila kati yao ilijua pahala pake makhsusi pa kunywa. Basi haikuwa huyu kumuingilia huyu. Na akajaalia kiwingu chende kuwapa kivuli chake katika jangwa, kuwakinga na mwako wa jua. Akawateremshia Manna, nacho ni chakula kwa sura kinafanana na mvua ya barafu, na tamu kama asali. Na akateremsha Salwa, naye ni ndege aliye nona. Na akawaambia: Kuleni hivi vinono tulivyo kuruzukuni katika tulivyo kuteremshieni. Lakini walijudhulumu nafsi zao, na wakazikufuru neema hizo, kwa kuzikataa na kutaka nyenginezo. Na Sisi hatukupata madhara kwa udhalimu wao, lakini upungufu wamepata wao.