Kisha Mwenyezi Mungu alimuamrisha awalete baadhi ya jamaa katika kaumu yake wawatakie radhi walio muabudu ndama, na akawapa miadi. Musa akawateuwa katika kaumu yake watu sabiini katika wasio muabudu ndama, nao wakawa wanawawakilisha kaumu yao. Akenda nao mpaka kwenye mlima. Na huko wakamwomba Mwenyezi Mungu awaondolee balaa, na akubali toba ya walio muabudu ndama kati yao. Ikawachukua zilzala (tetemeko) kubwa pahala hapo, wakazimia kwa sababu yake. Na hayo kwa kuwa hawakuwaacha kaumu yao walipo abudu ndama, wala hawakuamrisha mema, wala hawakuwakanya maovu! Musa alipoona yale alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Lau ungeli penda kuwaangamiza ungeli waangamiza kabla hawajaja hapa kwenye miadi, na ukaniangamiza na mimi pia, ili waone hayo Wana wa Israili wasinituhumu kuwa mimi nimewauwa. Basi ewe Mola Mlezi wangu! Usituhiliki kwa walio yafanya wajinga kati yetu. Kwani hii balaa ya kuabudu ndama haikuwa ila ni majaribio yaliyo toka kwako. Wewe unampoteza unaye taka apotee katika hao wanao ishika njia ya shari, na unawahidi (unawaonoza) unaye taka ahidike. Wewe ndiye mwenye kusema: Nitawaandikia wenye kujikinga na ukafiri na maasi katika kaumu yako, na akatoa Zaka iliyo faridhiwa, na Mwenye kusamehe madhambi.