Pamoja na hawa simulia kisa cha Maryamu aliye ulinda uke wake, nasi tukamfikishia siri katika siri zetu. Tukamjaalia achukue mimba bila ya mume, na tukamjaalia mwanawe azaliwe bila ya baba. Akawa yeye na mwanawe dalili iliyo wazi ya uweza wetu kugeuza sababu na vinavyo sabibishwa. Na hakika Sisi ni waweza wa kila kitu.
Hakika mila hii, nayo ndiyo Uislamu, ndiyo mila iliyo sahihi inayo kupasini kuilinda, kwa kuwa ni mila moja iliyo shikamana wala haikukhitalifiana baina ya hukumu zake. Basi nanyi msifarikiene katika mila hii kwa makundi na vyama. Na Mimi ndiye Muumba wenu, na Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Basi niabuduni Mimi tu, wala msinishirikishe na mwengine.
Na juu ya kuwepo uwongozi huu aghlabu ya watu wamegawanyika kwa mujibu wa matamanio yao, wakafanya mambo yao ya Dini mapande mapande, wakawa makundi mbali mbali. Na kila kundi litaturejea Sisi tulihisabie vitendo vyake.
Basi mwenye kutenda vitendo vyake vyema, naye ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Dini yake aliyo iridhia, hatopunguziwa kitu katika juhudi yake. Bali atalipwa malipo kaamili. Na Sisi ni wenye kuiandika hiyo juhudi yake. Basi hakitopotea kitu.
Na haitakuwa kwa watu wa mji tulio uteketeza kwa sababu ya dhulma yao kwamba hawatarejea kwetu Siku ya Kiyama, bali hapana budi kuwa watarejea na tutawahisabia vitendo vyao viovu.
Mpaka itapo funguliwa milango ya shari na ufisadi, wakaingia wana wa Juju na Maajuju wakikimbizana kuteremka milimani na majiani kwa kufanya vitendo vya fujo na rabsha.
Na ikakaribia miadi iliyo haina budi kutimizwa, nayo ni Siku ya Kiyama, wakawa wale walio kufuru wanakutikana wakikodoa macho yao kwa wingi wa kitisho, wakipiga makelele kusema: Kitisho gani hichi cha kutuangamiza! Hakika sisi tulighafilika na Siku hii. Bali tulikuwa ni wenye kujidhulumu nafsi zetu kwa ukafiri na inda.
Wataambiwa makafiri hawa: Nyinyi na hiyo miungu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Moto wa Jahannamu. Nyinyi mtaingia humo muadhibiwe!
Lau kama hawa mlio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni miungu inayo stahiki kuabudiwa, wasingeli ingia nanyi humo. Na nyote, wenye kuabudu na kuabudiwa, mtabaki Motoni, wala hamtatoka.
Hakika wale tulio wakubalia kwa kufuata kwao Haki na vitendo vya kheri, na tukawaahidi malipo mema, hao watawekwa mbali kabisa na Jahannamu na adhabu yake.