Anaye stahiki sifa njema ni Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye ndiye aliye zifanya mbingu na ardhi zikawa bila ya kuwapo ruwaza ya kuigia mfano wake. Naye ndiye aliye wajaalia Malaika kuwa ni wajumbe kuwatuma kwa viumbe vyake. Wao hao wana mbawa za idadi mbali mbali, mbili-mbili, tatu-tatu, na nne-nne. Yeye huzidisha katika kuumba kwake kama atakavyo kuzidisha. Hashindwi na kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa juu ya kila kitu.
Mwenyezi Mungu akipeleka rehema kwa watu, rehema yoyote ile iwayo, ikiwa ni mvua, au neema, au amani, au hikima - hapana mtu yeyote awezaye kuwazuilia na kuwanyima. Na chochote katika hivyo akikizuilia Yeye basi hapana mmoja awezaye kukifungulia isipo kuwa Yeye Mwenyewe. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi. Mwenye hikima asiye kosea.
Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu, kwa kuzishukuru na kutimiza haki yake. Na mkiri hayo yaliyo tokea ndani ya nafsi zenu, ya kwamba hapana muumba isipo kuwa Mwenyezi Mungu ambaye anakuruzukuni kutoka mbinguni kwa zinavyo viteremsha, na kutoka kwenye ardhi kwa vinavyo toka humo, ambavyo vinakuleteeni uhai wenu. Hapana mungu isipo kuwa Yeye anaye waruzuku waja wake. Basi yawaje mnavyo geuzwa mkaacha Tawhidi ya Muumba wenu na Mwenye kukuruzukuni mkaendea kumshirikisha katika ibada yake?