Isa akawaitikia, na akasema: Ewe Mola wetu Mlezi, uliye miliki mambo yetu yote! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni, kiwe ni siku-kuu kwetu kitapo teremka kwa walio amini miongoni mwetu, kwa walio tangulia na walio taakhari, na kiwe ni muujiza wa kutilia nguvu wito wako, na uturuzuku riziki njema, na Wewe ndiye Mbora wa kuruzuku.
Mwenyezi Mungu akamwambia: Mimi nitakuteremshieni chakula kutoka mbinguni. Lakini mtu yeyote atakaye pinga neema hii baada ya kuteremka, basi Mimi nitampa adabu ambayo sijapata kumpa mtu yeyote. Kwani huyo atakuwa anakanya baada ya kwisha shuhudia dalili ya Imani aliyo itaka mwenyewe.
Ewe Nabii! Taja yatakayo tokea Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu atapo mwambia Isa bin Maryamu kauli ya kutangaza haki: Ati wewe ndiye uliye waambia: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu, na muache kumuabudu Mwenyezi Mungu wa pekee? Isa atasema: Mimi ninakutakasa mtakaso wa ukamilifu ya kuwa Wewe huna mshirika. Wala hainifalii mimi nitake jambo ambalo sina haki nalo hata chembe. Lau kuwa nimesema hayo, basi Wewe ungeli jua. Kwani Wewe unayajua yaliyo fichikana ndani ya nafsi yangu, licha yanayo dhihiri kwa kuyasema. Wala mimi siyajui unayo nificha. Hakika Wewe ndiye Mwenye ujuzi ulio enea kila kilicho fichikana na kilicho ghibu. (Wakristo wote wanamuabudu Yesu, na Wakatoliki wanamwomba Maryamu pia, na wanamwita: "Mama wa Mungu")
Mimi sikuwaambia ila uliyo niamrisha niwafikishie. Nimewaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani Yeye ndiye Mwenye kumiliki mambo yangu na yenu. Na mimi nilikuwa naijua hali yao nilipo kuwa nao. Na ulipo malizika muda uliyo nikadiria nikae nao ulikuwa Wewe peke yako ndiye unaye wajua. Na Wewe ni Mwenye kujua kila kitu.
Ukiwaadhibu kwa waliyo yatenda basi hao ni waja wako, unawafanya upendavyo. Na ukiwasamehe, basi hakika Wewe peke yako ndiye Mtenda nguvu usiye shindwa, Mwenye hikima yenye kufikilia kila linalo toka kwako.
Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Watapata mabustani yanayo pitiwa na mito chini ya miti yake. Na humo watakaa, wala hawatatoka milele, wakistarehe humo kwa radhi ya Mwenyezi Mungu anavyo waridhia wao, na wao watavyo kuwa radhi kwa malipo alio walipa. Na Neema hiyo ndio kufuzu kukubwa.
Ufalme wa mbinguni na katika ardhi na vyote viliomo humo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye peke yake ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa, na Yeye tu ndiye Mwenye uweza ulio timia kutekeleza kila alitakalo.