Makafiri wanataka kwa madai yao ya upotovu waizime Nuru ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Uislamu. Na Mwenyezi Mungu hataki ila aitimize Nuru yake, kwa kuidhihirisha Dini yake na ashinde Mtume wake, ijapo kuwa wao watachukia.
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu aliye dhamini kutimiza Nuru yake kwa kumtuma Mtume wake, Muhammad s.a.w. na hoja zilizo wazi, na Dini ya Haki, Uislamu, ipate kutukuka Dini hii juu ya dini zote zilizo tangulia, ijapo kuwa washirikina watakasirika. Mwenyezi Mungu ataipa ushindi tu, wakitaka wasitake.
Enyi Waumini! Jueni kuwa wengi katika wataalamu wa Kiyahudi na mapadri wa Kikristo wanajihalalishia kula mali ya watu bila ya haki yoyote, na wanawazuga wafwasi wao wanao waamini kwa kila walisemalo. Na wanawazuilia watu wasiingie katika Uislamu. Na wale wanao kusanya mali, dhahabu na fedha, wakiyaweka tu, wala hawatoi Zaka zake, waonye ewe Mtume, kuwa kuna adhabu ya kutia uchungu _
-- Siku ya Kiyama, kwa kuwa hayo mali yatatiwa kwenye Moto wa Jahannamu, kisha waunguzwe nayo kwenye vipaji vya nyuso zao, na mbavu zao, na migongo yao; na waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkijilimbikia kama khazina kwa ajili ya nafsi zenu, wala hamkuwa mkitoa haki ya Mwenyezi Mungu! Basi ionjeni hii leo adhubu kali!
Hakika hisabu ya miezi ya kuandama ni miezi kumi na mbili, kwa hukumu na kudra ya Mwenyezi Mungu, na ndivyo alivyo ibainisha katika vitabu vyake tangu kuanza ulimwengu. Na katika hii miezi thinaashara (kumi na mbili) ipo mine imekatazwa kupigana vita ndani yake, nayo:-Mwezi wa Rajab, Alqa'ada (Mfungo Pili), Alhijja (Mfungo Tatu), na Almuharram (Mfungo Nne). Na huku kuitukuza miezi hii mine na kuharimisha kupigana vita ndani yake ndiyo Dini ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka, ambayo haibadiliki wala haina mageuzo. Basi msijidhulumu nafsi zenu kwa kuhalalisha vita katika miezi hii, au mkaacha kujilinda adui akikupigeni. Na enyi Waumini! Piganeni na washirikina bila ya kumbagua yeyote kati yao, kama wanavyo kupigeni nyinyi nyote. Na kuweni na yakini kuwa Mwenyezi Mungu atawanusuru wanao mcha, na wakashika amri zake, na wakaepuka anayo yakataza.