Na wengi katika watu wa miji tuliyo iteketeza kwa sababu ya ukafiri wao na kuwakadhibisha Manabii, na baada yao tukasimamisha kaumu nyengine zenye hali bora na mwisho mwema kuliko hao.
Na tulipo taka kuwateketeza, na wakahisi ukali wa adhabu yetu na uwezo wetu wa kuwateremshia hayo yatakayo wapata, wakafanya haraka kukimbia, kama wanyama hayawani, ati kutafuta kuokoka!
Enyi wapinzani! Msikimbie! Hapana kitu chochote kitacho kulindeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Rudini kwenye zile zile neema na majumba mliyo kuwa nayo, huenda watumishi wenu na wenzenu watakutakeni msaada na rai kama ilivyo kuwa ada yenu. Wapi! Hamtoweza!
Kwa kuwa hao makafiri wamekwisha sikia wanavyo kejeliwa na wanavyo itwa kwenda teketezwa na wana yakini nako, basi watasema: Hakika kweli sisi tulikuwa ni wenye kudhulumu tulipo yaacha yanayo tunafiisha, na tusiziamini Ishara za Mola wetu Mlezi.
Maneno hayo hawaachi kuyakariri na kuyapigia makelele mpaka kwa adhabu yetu tukawafanya kama mimea iliyo fyekwa, na moto ulio zimika, hawana tena uhai.
Wala hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mpango huu wa hikima, na muundo huu wa namna peke yake, kwa mchezo. Bali tumefanya yote haya kwa hikima ya juu ambayo wanaifahamu wenye kuzingatia.
Lau kuwa tunataka kufanya mchezo na pumbao isingeli mkinika kuchukua ila yaliyo katika ufalme wetu, kwani hapana ufalme ila wetu - ingeli kuwa Sisi ni wa kufanya hayo. Wala nasi si wenye kufanya hayo, kwa kuwa si laiki ya haki yetu.
Lakini jambo linalo tuelekea Sisi kulifanya ni kuipambanisha kweli juu ya uwongo ipate kuuondoa. Na nyinyi makafiri mtahiliki kwa sababu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Na ni vya Mwenyezi Mungu peke yake vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, kwa kuviumba na kuvimiliki. Basi ni haki Yeye peke yake kuabudiwa. Na Malaika walio karibishwa kwake hawana kiburi cha kuwazuia kumuabudu na kumnyenyekea, wala hawaoni machofu na kunyong'onyea kwa ibada ya mchana na usiku.
Washirikina hawafanyi wafanyavyo walio karibishwa katika kumsafishia ibada Mwenyezi Mungu, bali wao wamewaabudu wenginewe, na wakafanya miungu duniani isiyo stahiki kuabudiwa. Na huwaje kwenda kuabudu kitu kisicho kuwa Mwenyezi Mungu, ambacho hakiwezi kufufua?
Lau kuwa mbinguni na duniani kuna miungu isipo kuwa Mwenyezi Mungu wanao endesha mambo yao, basi ingeli haribika nidhamu iliyo simamishiwa hizo mbingu na ardhi kwa kuumbwa, na ikafikilia mwisho wa mpango na hikima. Basi na atakasike Mwenyezi Mungu, Mwenye Ufalme wote, na yote wanayo msingizia washirikina.
Yeye Subhanahu hahojiwi kwa anayo yatenda, kwani ni Yeye pekee mwenye utukufu na madaraka, Mwenye hikima na ujuzi. Hakosei katika kutenda chochote. Ni wao ndio watahisabiwa na kuhojiwa kwa wanayo yatenda, kwa kuwa wao hukosea kwa udhaifu wao na ujinga wao na kughilibiwa na matamanio.
Hawaujui waajibu wa Mwenyezi Mungu uliyo juu yao, ndio maana wakawa na miungu mingine isiyo kuwa Yeye wakaiabudu bila ya kuwa na ushahidi wowote wa kuingia akilini, wala uthibitisho wa kweli. Ewe Nabii! Waambie: Leteni uthibitisho wenu kama kweli Mwenyezi Mungu ana mshirika katika utawala hata akafaa kushirikishwa katika kuabudiwa. Hii Qur'ani iliyo kuja kuukumbusha umati wangu kwa linalo wajibikia, na hivi Vitabu vya Manabii wengine vilivyo kuja kukumbusha kaumu za kabla yangu, vyote hivyo vimesimama juu ya Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui yaliyo kuja ndani ya Vitabu hivyo, kwa sababu hawajishughulishi kuyazingatia yaliomo humo. Basi wao wamekuwa wenye kuipuuza Imani ya Mwenyezi Mungu.