Na katika kejeli zao kukufanyieni ni vile pale mnapo ita kwenda kuswali katika adhana, wao huifanyia maskhara Swala yenu, na hukuchekeni, wakafanya ni mchezo. Na hayo ni kwa sababu kuwa wao ni kaumu wasio na akili, wala hawatambui farka iliopo baina ya upotofu na uwongofu.
Sema ewe Mtume! Enyi Watu wa Kitbu! Hivyo mnatuchukia kwa kuwa tunamuamini Mwenyezi Mungu na tunaamini tuliyo teremshiwa sisi, nayo ni Qur'ani, na Vitabu vilio sahihi vilio teremshiwa Manabii wa zamani, na kwa kuwa tunaamini kuwa wengi wenu mmeitupa Sharia ya Mwenyezi Mungu?
Waambie: Nikwambieni malipo maovu kabisa kutokana na Mwenyezi Mungu? Ni hivyo vitendo vyenu nyinyi mlio tengwa mbali na Mwenyezi Mungu na rehema yake, na mkakasirikiwa kwa sababu ya ukafiri wenu na uasi wenu, na mkazibwa nyoyo zenu, mkawa kama manyani na nguruwe, na mkamuabudu Shetani, na mkafuata upotovu. Nyinyi ndio mko katika daraja ya mwisho katika shari, kwa sababu nyinyi ni watu walio potea kabisa, mkaiwacha Njia ya Haki.
Wanaafiki wakikujia husema uwongo, na hukwambia: Tumeamini. Nao wamekuingilia na hali ni makafiri, na wametoka kwenu nao ni makafiri vile vile! Na Mwenyezi Mungu anaujua vyema unaafiki wanao uficha. Na Yeye ndiye atakaye waadhibu.
Na utawaona wengi wao hawa wanakimbilia kufanya maasi na kuwatendea uadui wengineo, na pia katika kula mali ya haramu kama rushwa (mrungura) na riba! Uwovu gani huu wautendao!
Si ingelikuwa vyema lau kuwa wanazuoni wao na makohani wangeli wakataza kusema uwongo, na kula haramu? Uwovu mkubwa huo wanao ufanya kwa kuacha kusemezana na kukatazana maasi.
Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba, haukukunjuka ukatoa! Mwenyezi Mungu ameifumba mikono yao wao, na amewatenga mbali na rehema yake! Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, anajitosha. Yeye hutoa apendavyo. Na hakika wengi wa watu kwa kupita kiasi katika upotovu wao, haya yalio teremka kwako huwazidisha udhalimu na ukafiri, kwa sababu ya chuki na husda yao. Na Sisi tumetia baina yao kwa wao uadui na bughdha mpaka Siku ya Kiyama. Kila wanapo washa moto kumpiga vita Mtume na Waumini, Mwenyezi Mungu huuzima kwa kumpa ushindi Nabii wake na wafuasi wake. Na wao wanajitahidi kueneza fisadi katika nchi, na kufanya vitimbi, na kutia fitina, na kuchochea vita. Na Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.