Tungeli penda bila ya shaka tungeli kuonyesha hao wanaafiki, nawe ungeli wajua kwa alama zao, na ungeli wajua kwa namna yao wanavyo sema. Na Mwenyezi Mungu anajua ukweli wa vitendo vyenu vyote.
Na ninaapa: Bila ya shaka tutakujaribuni kama kukufanyieni mtihani, mpaka tuwajue Mujaahidina, wanao pigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, katika nyinyi, na wenye kuvumilia wakati wa shida na dhiki, na tuzijue khabari zenu za ut'iifu na maasi katika Jihadi na penginepo.
Hakika walio kufuru na wakazuia njia ya Mwenyezi Mungu, na wakenda kinyume na Mtume kwa inda na ukaidi, baada ya kwisha wadhihirikia uwongofu, hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote. Na Yeye atayabat'ilisha yote waliyo yatenda.
Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu katika aliyo kuamrisheni, na mt'iini Mtume kwa hayo anayo kuitieni, wala msivipoteze vitendo vyenu.
Hakika walio kufuru na wakazuia watu wasiingie katika Uislamu, kisha wakafa nao ni makafiri, basi Mwenyezi Mungu hatawasamehe.
Basi msijifanye wanyonge mbele ya maadui zenu mnapo kutana nao. Wala msiwatake suluhu kwa kuwaogopa, na hali nyinyi ndio mko juu, na ni wenye kushinda kwa nguvu za Imani. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi kwa nusra yake; na wala hatakupunguzieni malipo ya vitendo vyenu.
Hakika uhai wa dunia ni upotovu na udanganyifu. Na nyinyi mkiamini na mkaacha maasi, na mkafanya kheri, Mwenyezi Mungu atakupeni thawabu ya hayo, wala hakutakini mali yenu. Akikutakeni na akakushikilieni basi nyinyi mtafanya uchoyo, na chuki zenu zitaonekana kwa mnavyo yapenda mali.
Hivi mnaitwa mtumie katika njia ya Mwenyezi Mungu aliyo iamrisha. Kati yenu wapo wanao fanya ubakhili kutoa. Na mwenye kufanya ubakhili hamdhuru mtu ila nafsi yake. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye tajiri, hana haja ya mtu, na nyinyi ndio mafakiri wenye kumhitajia Yeye. Na mkiacha kumt'ii Mwenyezi Mungu basi atakubadilisheni pahala penu awalete watu wengine, tena hao hawatakuwa mfano wenu wa kuacha kumt'ii.