Enyi watu! Tanabahini na mjue ya kuwa wenye kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa Imani na ut'iifu Yeye anawapenda, na wao wanampenda. Hawana khofu ya kuhizika duniani, wala kupata adhabu ya Akhera. Wala wao hawahuzuniki kwa kukosa starehe za duniani, kwa kuwa watapata kwa Mwenyezi Mungu yaliyo makubwa na mengi kuliko hayo.
Kwa wapenzi hawa wa Mwenyezi Mungu pana bishara ya kheri hapa duniani, kwa vile Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwapa ushindi na utukufu, na Akhera itatimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haigeuki. Na haya ndiyo waliyo bashiriwa kwayo duniani, na watayapata Akhera. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
Ewe Mtume! Usihuzunuke kwa wayasemayo washirikina ya kejeli, na matusi, na kukadhibisha. Wala usidhani kuwa hali yao hii itadumu. Bali ushindi ni wako, na Uislamu utatukuka, kwani utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ushindi upo mkononi mwake, na Yeye atakunusuru uwashinde hao makafiri. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye kuyasikia wanayo kuzulia, na Mwenye kuyajua wanayo dhamiria. Na Yeye atawalipa kwa hayo.
Enyi watu! Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu peke yake vyote viliomo mbinguni na duniani, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kuviendesha. Na hao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu kwa hakika hawawafuati hao miungu ya ushirikina. Hao si chochote ila wanafuata mawazo tu, wanadhani kuwa uwezo umo katika vitu ambavyo havijifai wenyewe, la kwa manufaa wala madhara.
Hakika huyo Mwenye kumiliki viliomo katika mbingu na ardhi, ndiye aliye kuumbieni usiku mpate kupumzika na mahangaiko ya mchana. Na amekuumbieni mchana wenye kuangaza mpate kufanya kazi na mshughulikie maslaha yenu. Hakika katika kuumbwa usiku na mchana zipo dalili zilizo wazi kwa wenye kusikia na wakapima.
Na ikiwa wanao abudu masanamu wamefanya ushirikina wa kuabudu mawe, na hawakumtakasa Mwenyezi Mungu kwa haki ya kumtakasa, na wakasema kuwa Allah, Mwenyezi Mungu, ana mwana, basi Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo. Yeye hana haja ya kuwa na mwana; kwani kuwa na mwana kunaonyesha wazi kutaka kubakia ukoo wako baada ya kufa kwako. Na Mwenyezi Mungu hafi. Yeye ni Mwenye kubakia milele. Na vyote viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi ni vyake, vimeumbwa na vinaendeshwa na Yeye. Na nyinyi wazushi, hamna hoja yoyote wala dalili ya hayo mnayo zua! Basi msikhitalifiane juu ya Mwenyezi Mungu kwa mambo yasiyo na msingi wa hakika.
Wao wana starehe hapa duniani ya kudanganyika nayo. Nayo ni chache, ikiwa itachukua muda mrefu au mfupi, ukilinganisha na hayo yanayo wangojea! Kisha marejeo yao ni kwetu, Sisi. Tutawahisabia na tutawaonjesha adhabu ya kutia uchungu kwa sababu ya ukafiri wao.