Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni na maadui zenu mara nyingi katika vita kwa nguvu ya Imani yenu. Na mlipo ghurika na wingi wenu katika vita vya Hunayni, kwanza Mwenyezi Mungu alikuachieni wenyewe. Wingi wenu usikufaeni kitu. Adui akakushindeni, na kwa shida ya kufazaika mkaiona ardhi kuwa ni nyembamba. Msiweze kupata njia ya kupigana wala kuokoka kwa murwa. Wengi wenu wakawa hawana njia ya kuepuka ila kukimbia. Mkakimbia kwa kushindwa, na mkamuacha Mtume na Waumini wachache tu. Vita vya Hunayni walipigana Waislamu na kabila mbili za Thaqiif na Hawaazin. Jeshi la Waislamu lilifika kiasi ya watu elfu kumi na mbili, na makafiri walikuwa elfu nne. Nao walipigana kwa ukali kwa kuwa ilikuwa wakishindwa wao basi ibada ya masanamu itatoweka kabisa kwa Waarabu, kwani Makka ilikuwa ndio kwanza kwisha tekwa. Majeshi mawili yakapambana, Waumini kwa wingi wao, nao uliwapandisha kichwa; na wale makafiri na uchache wao wakali. Kwanza makafiri wakashinda kwa kuwa Waislamu walighurika kwa wingi wao wakajiona. Lakini mwishoe vita vikaishia kwa kushinda Waumini. Funzo la hapa ni kuwa wingi sio unao pelekea ushindi, lakini nguvu za kimoyo na imani.