Mwenyezi Mungu amewatenga mbali na rehema yake wale makafiri miongoni mwa Wana wa Israili, na haya yameteremka katika Zaburi juu ya Nabii wake Daud, na katika Injili juu ya Nabii wake Isa mwana wa Maryam. Na hayo ni kwa sababu ya uasi wao, kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu na kuzama kwao katika udhalimu na ufisadi.(Katika Zaburi Daud anawaapiza Mayahudi:"Wewe, Mungu, uwapatilize. Na waanguke kwa mashauri yao, Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, kwa maana wamekuasi Wewe." - Zaburi 5.10. Katika Injili Yesu anawalaani: "Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehannum?" - Mathayo 23.33.)
Mtindo wao ulikuwa kutoambizana. Hapana amkatazaye mwenzie kufanya uovu. Kufanya kwao uovu na kuacha kukatazana ni katika vitendo vinavyo chusha mno!
Utawaona wengi miongoni mwa Wana wa Israili hufanya urafiki na washirikina, mapagani, na wanawafanya hao ndio wenzi wao wakishirikiana katika kuupiga vita Uislamu! Kitendo hichi kiovu wanajirimbikizia wenyewe nafsi zao, waje kupata malipo yake kwa kupata ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na wapate kudumu milele katika adhabu ya Jahannamu.(Hayo yalikuwa zama za Mtume s.a.w. na mpaka hii leo. Mayahudi wanatafuta kila rafiki ambaye atauvunja Uislamu, ilhali yafaa wawaone Waislamu ndio wa karibu mno nao, kwa kuwa wanaamini Mungu Mmoja na wanaamini Manabii wao wote.)
Na lau kuwa itikadi yao ni sawa kama inavyo faa iwe kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake Muhammad s.a.w., na Qur'ani aliyo teremshiwa, basi wasingeli wafanya makafiri kuwa ni wenzao kuwapinga Waumini. Lakini wengi miongoni mwa Wana wa Israili ni maasi, wameacha dini.
Ewe Nabii! Tunakuhakikishia ya kwamba utaona hapana watu wanao kuchukia na kukubughudhi wewe na wanao kuamini kama Mayahudi na hawa wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada. Na utawakuta walio karibu mno nawe kwa mapenzi ni wafwasi wa Isa, walio jiita wenyewe "Manasara". Kwa sababu wamo miongoni mwao makasisi wanao ijua dini yao, na marahibu (mamonaki) wat'awa, wanao mcha Mola Mlezi, na kuwa wao hawana kiburi cha kuwazuia wasisikie Haki. (Na haya yameonakana kuwa Waislamu wengi duniani asili yao walikuwa Manasara, Wakristo. Wao wakisha pata fursa ya kuufahamu Uislamu huufuata, lakini ni wachache miongoni mwa Mayahudi walio silimu. Kinacho wazuia ni kiburi. Lakini walio silimu basi wamekuwa Waislamu wakubwa.)
Na pia miongoni mwa Manasara wakiisikia Qur'ani aliyo teremshiwa Mtume huathirika nayo, macho huwatiririka machozi, kwa kuwa wanajua kuwa wanayo yasikia ni kweli tupu, basi nyoyo zao humili kwayo, na ndimi zao huomba dua kumwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Tumekuamini Wewe na Mitume wako, na Haki ulio wateremshia. Basi ipokee Imani yetu, na utufanye miongoni mwa Umma wa Muhammad ulio wafanya mashahidi na hoja kwa watu wote Siku ya Kiyama.