Wanaume wanalo fungu lao katika mali waliyo yaacha kurithiwa wazazi wawili na jamaa walio karibia. Na wanawake, aidha, wana fungu lao, bila ya kunyimwa au kupunjwa. Na mafungu hayo yamethibiti, na yamefaridhiwa, na yamekadiriwa, yakiwa mali yenyewe kidogo au mengi.
Na pindi ikiwa wamehudhuria wakati ule wa kugawanya urithi baadhi ya jamaa ambao hawarithi, na ni mayatima na masikini, basi wakirimuni kwa kuwapa chochote katika huo urithi ili kuzipoza nafsi zao, na kuondoa uhasidi katika nyoyo zao. Na ni vizuri pia katika kuwapa kuleta maneno laini na udhuru mwema.
Watu watahadhari na kuwadhulumu mayatima, na wawaogopee watoto wao wanyonge wasije na wao wakadhulumiwa kwa watendavyo wazee kwa mayatima wa watu wengine. Na wamwogope Mwenyezi Mungu katika kuwatendea mayatima. Na waseme maneno yaliyo kaa sawa yanayo fuata haki, wala wasimdhulumu yeyote.
Hakika wanao wadhulumu mayatima kwa kuchukua mali yao bila ya haki, hakika wanakula yatakayo wapelekea Motoni. Na Mwenyezi Mungu atawaadhibu Siku ya Kiyama kwa moto mkali wenye kutia machungu.(Je, huwaje basi adhabu ya mwenye kudhulumu mali ya Mwenyezi Mungu? Wakfu za misikiti, madrasa n.k.? Na huwaje mwenye kuuwa ili apate kudhulumu mali ya mayatima wa hao alio wauwa?)
Mwenyezi Mungu anakuamrisheni katika mambo ya kuwarithisha watoto wenu na wazazi wenu, pindi mtakapo kufa, kwa njia inayo leta uadilifu na maslaha. Nayo ni kuwa sehemu ya mwanamume ni sawa na sehemu ya wanawake wawili, ikiwa watoto wanao rithi ni wanaume na wanawake. Ikiwa watoto wote ni wanawake watupu, na idadi yao imezidi wawili, basi sehemu yao ni thuluthi mbili za tirka, yaani mali yaliyo achwa na maiti. Inafahamika katika madhumuni ya Aya kuwa fungu la binti wawili ni kama fungu la walio zidi hapo. Na akiwa mtu amemuacha binti mmoja tu, basi fungu lake ni nusu ya alicho kiacha. Na akiwa mtu amemuacha baba na mama, basi kila mmojapo kati ya hao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita, ikiwa huyo maiti alikuwa na mtoto mmoja - mwanamume au mwanamke - pamoja na hao wazazi wake. Akiwa hana mtoto na wakamrithi wazazi wake tu, basi mama sehemu yake ni thuluthi, na kilicho baki ni cha baba. Na ikiwa huyo maiti alikuwa na ndugu, basi mama yake atapata sudusi na kilicho baki ni cha baba, na wale ndugu hawapati chochote. Mafungu hayo hupewa wanao stahiki baada ya kwisha lipwa deni lilio kuwa juu ya maiti, na kutimiza yale aliyo yausia katika mipaka aliyo ruhusu Mwenyezi Mungu. Hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na huu ndio uadilifu na ndio hikima. Na nyinyi hamjui ni nani kwenu mwenye manufaa zaidi kwenu, baina ya wazazi na wana. Na kheri khasa ni aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuyajua maslaha yenu, na ndiye Mwenye hikima katika yale aliyo kulazimisheni.