Kwa huku kushindwa kwa muda, Mwenyezi Mungu anawasafisha jamaa Waumini, na anawat'ahirisha kutokana na wale wenye nyoyo mbaya na imani dhaifu, na wenye kueneza moyo wa kushindwa na wasiwasi; na kwa hivyo ndio anaung'olea mbali ukafiri na makafiri wenyewe pia.
Enyi Waumini! Msidhani kuwa mtaingia Peponi bila ya kubainika kati yenu wepi Mujahidiina, Wapigania Haki, wenye kusubiri na kuvumilia ambao wanat'ahirishwa na misukusuko na shida.
Nyinyi mlikuwa mkitaka kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kabla hamjayaona mauti na mkajua kitisho chake. Sasa basi nyinyi mmekwisha yaona mauti walipo uliwa ndugu zenu mbele yenu nanyi mnaangalia.
Katika vita vya Uhud ulitoka uvumi kuwa ati Mtume Muhammad s.a.w. kauwawa. Baadhi ya Waislamu walidahadari wakaingiwa kiwewe wakataka kurtadi, kuuacha Uislamu. Mwenyezi Mungu aliwakaripia kwa kuwaambia: Muhammad si chochote ila ni Mtume tu, na kabla yake wamekufa Mitume mfano wake yeye. Naye atakufa kama walivyo kufa wao, na atapita kama wao walivyo pita. Je, akifa au akauliwa ndio mtarejea nyuma kwenye ukafiri wenu? Na mwenye kurejea kwenye ukafiri baada ya kwisha amini, basi hatomdhuru kitu Mwenyezi Mungu, ila atakuwa anajidhuru nafsi yake kwa kujipeleka kwenye mateso. Na Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema wale wenye kusimama imara juu ya Uislamu, wenye kuishukuru neema yake.
Hayumkini mtu kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye amekwisha viandikia viumbe ajali yao. Na atakaye starehe ya dunia Mwenyezi Mungu atampa, na atakaye malipo ya Akhera atayapata. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao shukuru neema yake wakamt'ii kwa aliyo waamrisha ikiwa ni kupigana Jihadi au mengineyo.
Na Manabii wangapi wamepigana vita na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi kwa Mola wao Mlezi! Nyoyo zao hazikuingia woga, wala azma zao hazikudahadari, wala hawakuwanyenyekea maadui zao kwa sababu ya masaibu yaliyo wapata katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu. Haya ni kwa sababu wamo katika ut'iifu wake, na Mwenyezi Mungu huwalipa wanao vumilia ikiwafika balaa.
Na kauli yao vilipo kuwa vita vikali haikuwa ila kusema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu kubwa na ndogo. Na tusimamishe imara katika midani za vita, na utunusuru na hawa maadui wa Dini yako, wenye kukukanya Wewe na ujumbe wa Mtume wako.
Mwenyezi Mungu akawapa ushindi na tawfiqi katika dunia, na akawadhaminia malipo mema kwa Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwalipa wale wafanyao vitendo vyema.