Lakini wakakakamia katika ukhalifu wao. Wakasema: Ewe Musa! Sisi bila ya shaka yoyote tumekwisha azimia kuwa hatutaingia nchi hii kabisa, maadamu wamo hao majabari. Basi tuache na yetu; kwani wewe huna madaraka yoyote juu yetu. Nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane nao hao majabari. Sisi tutakaa hapa hapa hatubanduki.
Hapo tena Musa akamrejea Mola wake Mlezi akisema: Mola wangu Mlezi! Sina madaraka ila juu ya nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tuhukumie baina yetu na hawa watu wakaidi.
Mwenyezi Mungu akamuitikia Musa, akawapigia marfuku hao wakhalifu wasiingie nchi hiyo kwa muda wa miaka arubaini, wakipotea ovyo majangwani hawajui wendako wala watokako. Mwenyezi Mungu akamwambia Musa kama kumuasa: Usisikitike kwa masaibu yaliyo wasibu, kwani hawa ni wapotovu, wameiasi amri ya Mwenyezi Mungu.
Hakika kupenda kutenda uadui ni tabia ya baadhi ya watu. Basi ewe Nabii! Wasomee Mayahudi - na wewe ni msema kweli - khabari za Haabila na Qaabila, wana wawili wa Adam. Kila mmoja alichinja dhabihu kama ni mhanga kwa kutaka kuruba kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu alimkubalia mmoja kwa ajili ya usafi wa niya yake, na akamkatalia wa pili kwa kuwa niya yake haikuwa safi. Basi yule aliye kataliwa akamhusudu mwenzie na akamuahidi kuwa atamuuwa. Yule nduguye akamrudi kwa kumbainishia kuwa Mwenyezi Mungu hapokei a'mali ila kwa wachamngu walio safisha niya zao katika kule kutafuta kuruba.
Akamwambia: Shetani akikuzuga hata ukaninyooshea mkono ili kuniuwa, mimi sitofanya kama hivyo, wala sitanyoosha mkono wangu kwa ajili ya kukuuwa. Hakika mimi naogopa adhabu ya Mola wangu Mlezi, naye ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Mimi sitakuzuia utapo taka kuniuwa ili upate kubeba dhambi za kuniuwa mimi pamoja na dhambi zako za tangu hapo za kutomsafia niya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo wewe unastahiki huko Akhera kuwa katika watu wa Motoni. Na hayo ni malipo ya haki ya Mwenyezi Mungu kumlipa kila mwenye kudhulumu.
Basi nafsi yake ilimsahilishia kukhalifiana na maumbile, kumuuwa nduguye, akamuuwa. Kwa hivyo akawa kwa mujibu wa hukumu ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa walio khasiri, kwa kuwa ameipoteza imani yake na amempoteza nduguye.
Baada ya kumuuwa yakamjia majuto na kubabaika. Akawa hajui amfanyeje maiti! Mwenyezi Mungu akampeleka kunguru akafukua udongo amzike kunguru mwengine aliye kufa, ili amfunze muuwaji vipi kumsitiri mwenzake aliye kwisha kufa. Alipo hisi uovu wa aliyo yatenda, alijuta kwa ukhalifu wake, akasema: Nimeshindwa hata kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Akawa basi miongoni wa walio juta kwa makosa yake, na kwenda kinyume na yanavyo takikana na maumbile.