Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, kwa kuukubali Upweke wake, kisha wakasimama sawa sawa juu ya sharia zake, Malaika watawateremkia mara kwa mara wakiwaambia: Msikhofu kukuteremkieni shari, wala msihuzunike kuwa mtakosa kheri, na furahini kuwa mtapata Pepo mliyo ahidiwa kwa ndimi za Manabii na Mitume.
Na Malaika watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Na Malaika watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Hapana mwenye kauli nzuri zaidi kuliko mwenye kulingania Tawhid ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake, na pamoja na hayo, akatenda vitendo vyema, na akasema kwa kuungama itikadi yake: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu, yaani wenye kunyenyekea amri za Mwenyezi Mungu.
Haziwezi kuwa sawa tabia njema na tabia mbovu. Pinga uovu ukikujia kutokana na adui kwa tabia iliyo bora kuliko yake. Hapo matokeo yake ni huyo ambaye uliye kuwa na uadui naye atakuja kuwa kama mwenzio wa kukunusuru mwenye moyo safi.
Na hawaruzukiwi tabia hii, ya kulipa wema kwa uovu, ila wale wenye khulka ya kusubiri, na hawaruzukiwi hayo ila wenye fungu kubwa la tabia ya wema na ukamilifu wa nafsi.
Na akitokea Shetani akakutia wasiwasi kukuachisha hayo uliyo amrishwa, ewe unaye semezwa, basi jilinde naye kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu kusikia kwake na kujua kwake kumezunguka kila kitu. Na Yeye atakulinda naye.
Na katika dalili za uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni huu usiku na mchana, na jua na mwezi. Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo ni katika Ishara zake tu. Bali msujudieni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake, aliye umba jua, na mwezi, na usiku, na mchana, ikiwa nyinyi kweli mnamuabudu Yeye peke yake.
Ikiwa washirikina watajiona wakubwa hawafai kufuata amri yako, basi wewe usiudhike. Kwani hao walio kwa Mola wako Mlezi kwenye utakatifu wake, nao ni Malaika, wanamtakasa Yeye na kila upungufu katika kila wakati, usiku na mchana, wakimsafia ibada Yeye tu, wala hawachoki kumsabihi.