Na hao maadui wa Mwenyezi Mungu wakaziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Na ngozi zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu aliye tamkisha kila kitu. Na Yeye ndiye aliye kuumbeni hapo mwanzo kabla hamjawa chochote. Na kwake Yeye, peke yake, ndio mtarejea baada ya kufufuliwa, akuhisabieni mliyo kwisha yatanguliza katika vitendo.
Wala nyinyi hamkuwa mkiweza kuficha vitendo vyenu viovu hata viungo vyenu visivione na ikawa macho yenu, na masikio yenu na ngozi zenu, vyote hivyo vikakushuhudilieni. Lakini nyinyi mlikuwa mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hajui mengi katika vitendo vyenu, kwa sababu mkivifanya kwa uficho.
Lakini dhana mbovu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi imekuhilikini, na kwa hivyo mmekuwa Siku ya Kiyama katika wenye kukhasiri vibaya mno.
Basi hata wakijizuia machungu yao, Moto ndio mwisho wao, na makaazi yao ya daima. Na wakitaka kumridhi Mwenyezi Mungu sasa hawakubaliwi hayo matakwa yao.
Nasi tumewaandalia duniani marafiki waharibifu, na wao wakawazainishia mbele yao mambo ya Akhera, basi wakawaghuri kwamba ati hakuna kufufuliwa wala kuhisabiwa, na wakawapambia pia mambo ya duniani ili wastarehe nayo. Na neno la adhabu lilio wapata mataifa yaliyo kwisha pita miongoni mwa majini na watu walio kuwa kama wao, likawathibitikia na wao kwa sababu ya kukhiari kwao upotovu badala ya uwongofu. Hakika watu hao wote walikuwa katika walio khasiri khasara iliyo timia.
Makafiri wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Msiisikilize hii Qur'ani, na inapo somwa nyie leteni porojo lisio kuwa na maana, ili pasiwepo mtu wa kuisikia wala kunafiika kwayo, asaa kwa hivyo mkamshinda Muhammad.
Tunaapa: Bila ya shaka tutawaonjesha walio kufuru adhabu kali kwa vitendo vyao, na khasa kwa hivi kuipiga vita Qur'ani. Na bila ya shaka tutawalipa malipo maovu kabisa kwa vitendo vyao.
Hizo adhabu zilizo tajwa ni malipo wanayo stahiki maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto walio andaliwa katika makaazi ya kuishi milele, kuwa ni malipo kwa kule kuzikataa mfululizo Ishara za Mwenyezi Mungu na hoja zake.
Na makafiri watasema, nao wamo Motoni: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe hayo makundi ya majini na watu walio tupoteza ili tuwaweke chini ya nyayo zetu, wawe katika watu wa chini kabisa.