Ewe mwenye akili! Huyaangalii yaonekanayo kwa macho ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukaona anavyo wasahilishia watu wote kunafiika na ardhi na viliomo ndani yake? Na akawatengenezea bahari za kwendea ndani yake marikebu kwa mujibu apendavyo Yeye? Na akazishika sayari zote ziliomo angani kwa kudra yake hata zisikosee mpango wake, au zikaangukia kwenye ardhi, isipo kuwa akitaka kwa mapenzi yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliye takasika ni Mwingi wa huruma na rehema kwa waja wake. Kwa hivyo amewatengenezea kila njia za maisha mema. Huwaje basi baada ya haya yote hamumsafii niya Yeye kwa kumshukuru na kumuabudu? "Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu." Aya hii tukufu inakusanya maana za kisayansi za ndani. Mbingu, nayo ni kila kilicho juu yetu, inaanza kwa kuifunika ardhi kwa hewa, tena kwa anga, tena kwa vyombo vya mbinguni vinavyo toa mwanga kama nyota n.k. na visio toa mwanga wake mwenyewe kama mwezi, na sayari nyengine, na nyota mkia, na vumbi la ulimwengu, n.k. Vyote hivi vinakuwa vilivyo na vinashikana kwa athari ya nguvu mbali mbali. Muhimu wa hizo ni mvuto na nguvu inayo tokana na kule kuzunguka kwao. Yamedhihiri mapenzi ya Mwenyezi Mungu na huruma zake kwa waja wake kuwa katengeneza kifuniko cha angani kina namna za gasi mbali mbali ambazo ni dharura kwa uhai. Kama pia anawalinda wakaazi wa duniani na mianga na vimondo n.k. vinavyo zunguka angani na ambavyo vinapo karibia kwenye ardhi huungua kabla havijafika chini. Na katika mapenzi yake na rehema yake Mwenyezi Mungu ni kuwa hivyo vimondo vinavyo anguka kwenye ardhi ni nadra sana kutokea, na hutokea mwahala wasipo kaa watu. Jambo hili la dhaahiri laonyesha huruma na rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na haya yanatilia nguvu na kusadikisha kauli yake Mwenyezi Mungu: " na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu."
Na Yeye ndiye aliye kupeni uhai. Kisha anakufisheni unapo malizika muda wenu. Kisha tena atakufufueni Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo. Hakika mwanaadamu baada ya neema zote hizi na ushahidi wote huu ni mwingi wa kumkataa Mwenyezi Mungu na kuzikataa neema zake alizo mpa.
Tumewajaalia katika kila umma walio kwisha tangulia wawe na sharia zao makhsusi zinazo ambatana na zama zao, za kumuabudia Mwenyezi Mungu, mpaka zinapo kuja futwa na zijazo baadae. Na kwa hivyo tumewajaalia watu wako, ewe Nabii, wawe na Sharia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya Kiyama. Ilivyo kuwa hivi ndio amri yetu na mpango wetu, basi hao wanao jiabudia kwa dini zao zilizo pita, haiwafalii wao kutia mkazo katika kukupinga wewe. Kwani hakika sharia yako wewe imefuta sharia zao. Basi usijishughulishe na kujadiliana nao. Nawe endelea kuwaita watu wende kwa Mola wako Mlezi kwa mujibu wa unavyo pewa wahyi (ufunuo). Hakika wewe unafuata Uwongofu Ulio Nyooka wa Mola wako Mlezi.
Mwenyezi Mungu atahukumu baina yangu na nyinyi Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana nami. Atamlipa thawabu aliye ongoka na atamuadhibu aliye potoka.
Ewe mwenye akili! Jua kuwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu umekusanya kila kiliomo mbinguni na duniani. Hapana kitendo cha hawa washindani kinacho fichika kwake. Vyote hivyo vimekwisha andikwa katika Ubao ulio hifadhiwa (Lauhun Mahfuudh). Kwani kujua kwake Mwenyezi Mungu na kuvithibiti kwake ni kazi nyepesi kabisa kwake.
Na washirikina huabudu badala ya Mwenyezi Mungu masanamu na watu ambao haikuteremka hoja yoyote ya kuwaabudu hao katika Kitabu cha mbinguni chochote. Wala wao hawana ushahidi wowote wa kuingia akilini. Lakini wanafanya yote hayo kufuata pumbao na mila tu. Wala hao washirikina walio zidhulumu nafsi zao na wakazidharaulisha akili zao hawato pata msaidizi wa kuwanusuru, na kuwakinga na adhabu ya Moto Siku ya Kiyama, kama wanavyo jidai.
Ewe Nabii! Hawa washirikina mtu akiwasomea Aya zetu zilizo wazi, na ambazo ndani yake mna ushahidi wa ukweli wa hayo unao waitia, na ubaya wa ibada zao, utaona katika nyuso zao ghadhabu na chuki inayo wajaa, hata inakaribia kuwapelekea kutaka kumuuwa huyo anaye wasomea. Ewe Nabii! Waambie kwa kuwazindua na kuwaonya: Je! Mtanisikiliza nikwambieni yaliyo kuwa mabaya zaidi kuliko hiyo chuki inayo kuunguzeni roho? Ni Moto ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi walio kufuru kama nyinyi Siku ya Kiyama. Na hapana mwisho mbaya na makaazi maovu kuliko hayo.