Na kuweni wenye kumsafia niya Mwenyezi Mungu, wenye pupa kutaka kuifuata Haki, bila ya kumfuata mshirika wowote na Mwenyezi Mungu katika ibada. Kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu ameanguka huyo kutoka kwenye ngome ya Imani, na amesalitiwa na upotovu, na ameitia nafsi yake katika hilaki ya kutisha kabisa. Ikawa hali yake kama hali ya mtu aliye poromoka kutoka mbinguni na midege ikamrarua akakatika mapande mapande, asibakie hata alama. Au kama aliye peperushwa na upepo mkali, na mwili ukatawanyika mwahala mbali mbali.
Hakika mwenye kuitukuza Dini ya Mwenyezi Mungu na faridha ya Hija na a'mali zake na mihanga inayo pelekwa kwa ajili mafakiri wa Al-Haram, na wakachagua walio nona wazima, hawana ila, basi huyo ndio amemcha Mwenyezi Mungu. Kwani kutukuza kwake hayo ni matokeo ya unyenyekevu wa nyoyo zilizo amini, na alama katika alama za usafi wa niya.
Katika kutoa mihanga hii yapo manufaa ya kidunia. Mnawapanda na mnakunywa maziwa yake mpaka wakati wa kuwachinja. Kisha mnapata manufaa ya Kidini vile vile pale mnapo wachinja kwenye Nyumba Takatifu kwa kutafuta kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu.
Hizi faridha za Hija hazikukhusuni nyinyi peke yenu. Kwani tumewajaalia jamaa wote walio amini mambo ya kuwakaribisha kwa Mwenyezi Mungu, na wanataja jina lake, na wanamtukuza wakati wanapo chinja kwa kumshukuru kwa neema aliyo waneemesha, na kuwasahilishia wanyama wa mifugo, nao ni ngamia, ng'ombe, mbuzi na kondoo. Na Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni sharia nyinyi na wao ni Mungu Mmoja. Basi yasalimisheni mambo yenu yote kwake Yeye peke yake. Na vitendo vyenu visafisheni kwake, wala msimshirikishe na yeyote. Na ewe Nabii! Wape bishara ya Pepo na thawabu nyingi wale walio safisha niya zao kwa Mwenyezi Mungu na wakawa wanamnyenyekea Yeye miongoni mwa waja wake,
Wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hupapatika kwa kumkhofu, na hunyenyekea kwa kutajwa kwake, na ambao wanasubiri kwa masaibu ya karaha na shida yanayo wapata kwa kujisalimisha mbele ya amri yake na hukumu yake, na wakashika Swala kwa ukamilifu wake, na wakatoa baadhi ya mali aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu katika njia za kheri.
Nasi tumefanya uchinjaji ngamia na ng'ombe n.k. katika Hija kuwa ni katika matukuzo ya Dini yalio dhaahiri. Na nyinyi kwa hayo mnajileta karibu na watu. Nanyi katika hao mnapata kheri nyingi katika dunia kwa kuwapanda, na kunywa maziwa yake. Na Akhera mnapata malipo na thawabu kwa kuwachinja na kuwalisha mafakiri. Basi tajeni jina la Mwenyezi Mungu wakati mnapo wapanga kwa safu kwa ajili ya kuwachinja. Mkisha wachinja kuleni sehemu mkitaka, na walisheni mafakiri walio kinai hawaombi, na ambao wanalazimika kuomba kwa haja. Na kama tulivyo fanya kila kitu kiwe kit'iifu kwa tuyatakayo kwa ajili ya manufaa yenu, na tumedhalilisha hivyo vikut'iini nyinyi ili mpate kuishukuru neema yetu kubwa iliyo juu yenu.
Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu haangalii sura zenu wala vitendo vyenu, lakini anaangalia nyoyo zenu. Wala hataki kwenu mambo ya kujionyesha tu kwa kuchinja na kumwaga damu. Lakini anataka kwenu moyo wenye kunyenyekea. Basi hapati radhi yake mwenye kugawa hizo nyama wala damu. Lakini linalo pata radhi yake ni uchamngu wenu na usafi wa niya zenu. Kuwadhalilisha hao wanyama tulivyo wadhalilisha ni kwa ajili ya kukunafiisheni, mpate kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa vile alivyo kuongoeni hata mkatimiza ibada za Hija. Na ewe Nabii! Wape khabari njema watu wema walio tengeneza a'mali zao na niya zao kuwa watapata malipo makuu.
Hakika Mwenyezi Mungu huwalinda Waumini na huwahami na huwanusuru kwa Imani yao. Kwani Yeye hawapendi wenye kukhuni dhamana zao, wenye kupita mipaka katika ukafiri wao kumkataa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu hamsaidii yule asiye mpenda.