Katika kwenda vitani wao hubaki nyuma hawatoki nanyi kwenda kupigana na adui zenu wala hawataradadi. Na kisha hukutoleeni udhuru wa uwongo kwa kule kubaki kwao nyuma. Na hukuapieni ili muwaridhie na mkubali udhuru wao. Na wa kustahiki kutakiwa radhi kama wao kweli ni Waumini, ni Mwenyezi Mungu na Mtume.
Hivyo hawa wanaafiki hawajui kwamba malipo ya mwenye kumkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akashindana nao ni adhabu ya daima katika Moto wa Jahannamu? Na hiyo ndiyo hizaya ya kufedhehesha, na madhila makubwa.
Wanaafiki wanapo kuwa wao kwa wao humfanyia kejeli Mtume, na wao wanaogopa yasifedheheke mambo yao, zikamteremkia Nabii Aya za Qur'ani zitakazo fichua yale wanayo yaficha katika nyoyo zao, na wanayafanya ni siri baina yao! Ewe Mtume! Waambie: Fanyeni maskhara yenu mpendavyo, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyafichua hayo mnayo yaogopea yasije kudhihiri.
Ewe Mtume! Kuwa na yakini kwamba, baada ya kwisha fedheheka mambo yao hawa wanaafiki, ukawauliza sababu ya kuitia ila Dini na kumfanyia kejeli Mwenyezi Mungu na Ishara zake, wao hutoa udhuru kwa kusema: Tulikuwa tunapiga porojo na tukicheza tu! Waambie: Vipi inakufalieni kupiga porojo na kucheza kwa kumfanyia maskhara Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?
Msitoe udhuru kama huu wa uwongo! Ukafiri wenu umekwisha dhihiri baada ya kujidai kwenu kuwa mmeamini. Na ikiwa Sisi tutalisamehe kundi moja lenu lilio tubu na likaamini, kwa sababu ya kutubu kwake kwa kweli, na kuamini kwake, vile vile tutaliadhibu kundi jengine katika nyinyi kwa kushikilia kwake ukafiri na unaafiki, na ukhalifu wake katika haki ya Mtume na ya Waumini.
Wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake wamefanana kwa kuwa wote wanatenda maovu, na wanayaamrisha, na wanaiacha Haki na wanaikataza, na wanafanya ubakhili kutumia mali katika njia za kheri. Basi hao kama ni viungo vya mwili mmoja. Wamemwacha Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu naye akawaacha wala hawaongoi, kwa kuwa wao wamekwisha toka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu amewaandikia wanaafiki na makafiri Moto wa Jahannamu. Atawaadhibu humo, wala hawatatoka. Hayo yanatosha kuwa ni malipo yao, na pamoja na malipo hayo watapata kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu na adhabu ya daima Siku ya Kiyama.