Mwenyezi Mungu akampa adhabu kwa kauli yake ya mwisho, nayo ni vile kusema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi aliye mkubwa kabisa. Na akampa adhabu kwa kauli yake ya mwanzo, nayo ni kumkadhibisha Musa a.s.
Ujuzi wa hayo uko kwa Mola wako Mlezi tu, si kwa mwenginewe. (Nabii Isa a.s. ambaye Wakristo wanasema ni Mwana wa Mungu, au ndiye Mungu, pia anasimuliwa katika Biblia kuwa hakuijua Saa na Siku ya Kiyama. Injili ya Mathayo inanukulu maneno ya Yesu: "Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.")
Na wao siku watakayo iona hiyo Saa ya Kiyama ni kama kwamba hawakuishi duniani zaidi kuliko jioni moja tu, au mchana wake.