Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi Imani juu ya Imani yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima .
Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na awape adhabu wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanao mdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.