Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa.
Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia.
Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia.