Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na kuwasimamia.