Na tuliwakatia Wana wa Isrāīl bahari, wakapita kwa watu waliokuwa wamekaa na kuendelea kuabudu masanamu wao. Wana wa Isrāīl wakasema, «Tufanyie, ewe Mūsā, sanamu tupate kumuabudu na kumfanya mungu kama hawa watu walivyo na masanamu wanaowaabudu.» Mūsā akawaambia, «Hakika yenu nyinyi,enyi watu, ni wajinga wa kujua utukufu wa Mwenyezi Mungu, na hamjui kwamba ibada haifai kufanyiwa yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu.
Hakika hawa wanaowakalia hawa masanamu, ushirikina waliomo ndani yake umeangamizwa, na ni yenye kuangamiza na ni ya urongo yale waliokuwa wakiyafanya ya kuwaabudu masanamu hao ambao hawawazuilii adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia.
Mūsā akasema kuwaambia watu wake, «Je, niwatafutie muabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba na Akawatukuza juu ya walimwengu wa zama zenu kwa wingi wa Mitume watokanao na nyinyi, kumuangamiza adui yenu na kwa miujiza Aiyowahusu nayo.»
Na kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, neema zetu kwenu tulipowaokoa na kifungo cha Fir'awn na jamaa zake na unyonge na utwevu mliokuwa nao, wa kuchinjwa watoto wenu wa kiume na kuwaacha wanawake wenu ili watumike na wadharauliwe. Na katika kupitia kwenu mateso mabaya zaidi na maovu zaidi kisha kuwaokoa ni mtihani utokao kwa Mwenyezi Mungu kwenu na neema kubwa.
Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Alimpa ahadi Mūsā ya kuzungumza na Mola wake masiku thelathini, kisha Akamuengezea muda wa masiku kumi baada yake, ukakamilika wakati ambao Mwenyezi Mungu Alimuwekea Mūsā wa kusema na Yeye kuwa masiku arubaini. Na Mūsā alisema kumwambia ndugu yake Hārūn, alipotaka kwenda kuzungumza na Mola wake, «Kuwa ni badala yangu kwa watu wangu mpaka nitakaporudi, na uwahimize wamtii Mwenyezi Mungu na wamuabudu, na usifuate njia ya wale ambao wanaleta uharibifu katika ardhi.»
Na alipokuja Mūsā kwa wakati uliowekwa nao ni muda wa masiku arubaini na Akasema na yeye Mola wake kwa kumpa wahyi wake, maamrisho Yake na makatazo Yake, alifanya hamu ya kumuona Mwenyezi Mungu akataka amtazame. Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Hutoniona!»Yaani hutaweza kuniona ulimwenguni. «Lakini liangalie jabali, likitulia mahali lilipo nitakapolitokezea, basi utaniona.» Alipojitokeza Mola wake kwa lile jabali alilifanya lipondeke liwe sawa na ardhi. Hapo Mūsā alianguka akiwa amezimia. Alipopata fahamu kutoka kwenye hali ya kuzimia alisema, «Kwa kukutakasisha, ewe Mola wangu, na kila sifa isiyolingana na utukufu wako, mimi natubia kwako kutokana na kuomba kwangu kukuona katika uhai huu wa kilimwengu, na mimi ni wa mwanzo wa wenye kukuamini miongoni mwa watu wangu.»