Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuafukia aikubali haki, Anakikunjua kifua chake kukubali Imani na upweke wa Mwenyezi Mungu; na yule ambaye Anataka kumpoteza , Anakifanya kifua chake kiwe katika hali ya dhiki kubwa na kukunjika katika kuukubali uongofu, kama hali ya anayepaa kwenye tabaka za anga za juu, hapo akapatwa na uzito mkubwa wa kuvuta pumzi. Na kama anavyovifanya Mwenyezi Mungu vifua vya makafiri vibanike sana na kukunjika, hivyo basi ndivyo Atakavyowapatia adhabu wale wasiomuamini.
Na haya tuliliyokubainishia, ewe Mtume, ndio njia inayofikisha kwenye radhi za Mola Wako na Pepo Yake. Tumezifunua wazi hoja kwa yule anayekumbuka miongoni mwa wenye akili zilizokomaa.
Wale wanaokumbuka watapata mbele ya Mola wao, Aliyetukuka na kuwa juu, Siku ya Kiyama Nyumba ya Salama na Amani, isiyo na makero, nayo ni Pepo. Na yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuwanusuru na kuwalinda; hayo yakiwa ni malipo kwao kwa matendo yao mema.
Na kumbuka, ewe Mtume, ile Siku Atakayowakusanya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, makafiri na wategemewa wao, miongoni mwa mashetani wa kijini, na kuwaambia, «Enyi mkusanyiko wa majini, hakika mumewapoteza binadamu wengi.» Na watasema wategemewa wao miongoni mwa makafiri wa kibinadamu, «EweMola wetu, kila mmoja katika sisi amenufaika na mwengine, na tumefikia kikomo ambacho umekiweka kwetu kwa kumalizika uhai wetu wa duniani.» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema Awaambie, «Moto ndio mashukio yenu, mtakaa milele, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Ametaka asikaye milele,» miongoni mwa walioasi wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake na utengenezaji Wake, ni Mjuzi mno wa mambo yote ya waja Wake.
Na kama tulivyowapa uwezo mashetani wa kijini juu ya makafiri wa kibinadamu wakawa ni wategemewa wao, hivyohivyo tunawapa uwezo madhalimu wa kibinadamu juu ya wenyewe kwa wenyewe duniani kwa sababu ya maasia wayafanyayo.
Enyi majini na binadamu mlio washirikina, kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu- Maandiko yanaonesha kuwa Mitume wanatoka kwa wanadamu tu.[4]- wanaowapa habari za alama zangu zilizo wazi, zinazokusanya maamrisho na makatazo, zinazofafanua kheri na shari na wanaowaonya kukumbana na adhabu yangu Siku ya Kiyama? Watasema washirikina hawa, maijini na binadamu, «Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu kwamba Mitume wako wametufikishia aya zako na wametuonya makutano ya Siku yetu hii, na sisi tukawakanusha.» Na hawa washirikina, liliwadanganya wao pambo la maisha ya dunia. Na walizishuhudilia nafsi zao kwamba wao walikuwa wakiukataa upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakiwafanya warongo Mitume Wake, amani iwashukie.
[4]Hii ndio kauli yenye nguvu ya maimamu wa nyuma na waliokuja baada yao. Na hii 1 aya si dalili wazi ya kuwa kuna Mitume wa kijini. Angalia Tafsiri ya lbn Kathīr katika kusherehi aya hii.