Kwa hakika Waumini kikwelikweli ni wale ambao Wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazitumia sheria Zake, na wakiwa wapo pamoja na Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika jambo ambalo amewakusanya kwalo la maslahi ya Waislamu, hawaondoki mpaka wamuombe ruhusa. Kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa, ewe Nabii, ndio wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kikweli. Basi wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya haja zao, mruhusu unayemtaka miongoni mwa wale waliokuomba ruhusa kuondoka kwa udhuru, na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake wenye kutubia, ni mwingi wa huruma kwao.
Msiseme, enyi Waumini, mnapomuita Mtume wa Mwenyezi Mungu, «Ewe Muhammad!» wala «Ewe Muhammad bin Abdillah!» kama wanavyosema hivyo baadhi yenu kuwaambia wengine. Lakini mtukuzeni na mseme, «Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!» Kwa kweli Mwenyezi Mungu Anawajua wale wanaoondoka kutuka kwenye kikao cha Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa siri, bila ya ruhusa yake, wakisaidiana kujificha. Basi na wajihadhari wanaoenda kinyume na amri Yake wasije wakashukiwa na janga na shari au adhabu yenye uchungu iumizayo.
Jueni mtanbahi kwamba ni vya Mwenyezi Mungu vilivyoko mbinguni na ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki, kuvifanya vimdhalilikie. Ujuzi Wake umevizunguka vyote ambavyo muko navyo. Na Siku ya Akhera, ambayo waja watarejea Kwake, Atawapa habari ya matendo yao, na Atawalipa kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, hayafichamani Kwake Yeye matendo yao na hali zao.