Basi wenye kujadiliana nawe, ewe Nabii, katika shani ya Isa baada ya kukujia wewe khabari iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu na ambayo haina ubabaifu ndani yake, basi waambie kauli itakayo dhihirisha ujuzi wako wa yakini na upotovu wao wa uwongo: Njooni! Kila mmoja wetu na wenu awaite watoto wake, na wakeze na wenyewe nafsi zao. Kisha tumnyenyekee Mwenyezi Mungu kumtaka ateremshe ghadhabu yake na nakama yake juu ya aliye mwongo katika hili jambo la Isa kuzaliwa bila ya baba na kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu wala si Mwana wa Mungu.