Na Mwenyewe Subhana ameeleza kuwa lazima watapata madhila popote watapo kutikana, ila wakifungamana kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Waislamu. Na wao wamestahiki wapate ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pia Mwenyezi Mungu amewajaalia lazima uwafikie unyonge na unyenyekevu kwa wengineo. Na hayo ni kwa sababu ya kukataa kwao Ishara zote za Mwenyezi Mungu zinazo onyesha Unabii wa Muhammad s.a.w. na vile kuridhi kwao hapo zamani kuuliwa Manabii ambako hakuwezi kuwa ni kwa haki, bali ni kwa uasi wao na uadui wao.