Enyi watu! Sisi tunakufahamisheni ukweli wa ajabu, basi hebu usikilizeni na muuzingatie. Haya masanamu hayataweza kabisa kuumba chochote hata kikiwa kitu duni kabisa kama nzi; hata ikiwa yote yakisaidiana katika kuumba huko. Bali huyu makhluku duni kabisa akiwanyang'anya chochote katika hizo sadaka wanazo pewa masanamu hawawezi kumzuia au kumfukuza. Unyonge gani basi huo wa kushindwa na nzi kutoweza kurejesha alicho pokonya. Na nzi ni kitu dhaifu mno! Wote wawili ni wanyonge. Bali hayo masanamu ambayo kama mnavyo ona ni dhaifu zaidi, basi huwaje mwanaadamu mwenye akili akenda kuyaabudu na kutaka yamnafiishe.
Hawa washirikina hawamjui Mwenyezi Mungu kama anavyo faa kujuulikana, wala hawamtukuzi kama anavyo stahiki kutukuzwa, walipo kwenda kumshirikisha katika ibada na vitu visio kuwa na maana kabisa. Na hali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muweza wa kila kitu, Asiye shindika na yeyote.
Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hikima yake yamempelekea kuteuwa Wajumbe kutokana na Malaika, na kutokana na wanaadamu, ili wafikishe sharia yake kwa viumbe vyake. Basi huwaje mkampinga aliye mchagua Mwenyewe kuwa ni Mjumbe wake kwenu? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia wayanenayo waja wake, Mwenye kuviona vitendo wavitendavyo. Naye atawalipa kwavyo.
Na Yeye Subhanahu anajua hali zao zilizo dhaahiri na za ndani. Hapana kinacho fichika kwake. Na kwake Yeye pekee ndiyo yanarejea mambo yote.
Enyi mlio amini! Msishughulikie upotovu wa makafiri. Nyinyi endeleeni na kutimiza Swala zenu kwa ukamilifu kwa kurukuu na kusujudu. Na muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni na akakuruzukuni. Wala msimshirikishe naye na yeyote. Na tendeni kila lenye kheri na manufaa, ili mpate kuwa watu wema, walio bahatika katika Akhera yenu na dunia yenu.
Na wanieni katika Jihadi ya kunyanyua Neno la Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi zake mpaka mwashinde maadui zenu na myashinde matamanio yenu. Kwani Yeye Subhanahu amekukaribisheni kwake, na amekuteueni muinusuru Dini yake, na amekujaalieni muwe Umma wa katikati. Wala hakukulazimisheni katika aliyo kuwekeeni Sharia lolote lenye mashaka juu yenu msilo weza kulichukua. Na amekufanyieni mepesi katika yanayo kuleteeni mashaka, na katika msiyo yaweza amekufanyieni ruhusa namna mbali mbali. Basi ishikeni Dini hii, kwani hii ndiyo Dini ya baba yenu Ibrahim katika misingi yake. Na Yeye Subhanahu ndiye aliye kuiteni Waislamu, (yaani Wanyenyekevu) katika Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia, na pia katika hii Qur'ani kwa ut'iifu wenu kwa yale aliyo kutungieni sharia. Basi kueni kama alivyo kuiteni Mwenyezi Mungu ili muwe mwisho wenu mnamshuhudia Mtume kama amekufikishieni ujumbe nanyi mkatenda aliyo kufikishieni, mpate kufanikiwa, na muwe mashahidi kwa kaumu zilizo tangulia kwa yaliyo kuja katika Qur'ani kwamba Mitume wao nao walifikisha ujumbe. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu amekuchagueni nyinyi khasa kuwa ni wat'iifu kwake, mkashika Swala kwa ukomo wa ukamilifu wake, basi ni waajibu wenu kulipa hayo kwa kumshukuru na kumt'ii, mshike Swala kwa utimilifu wake, na mwape Zaka wanao stahiki, na mumtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote, na mchukue kwake msaada, kwani Yeye ndiye Msaidizi wenu na ndiye wa kuwanusuru. Yeye ndiye Mbora wa ulinzi na Mbora wa kunusuru.