Haiwajii Qur'ani kutokana na Mola wao Mlezi pale inapoteremka kuwakumbusha ya kuwanufaisha, ila wao huisikiliza na hali wao wameshughulika na mengine yasiyo na faida nao, wakicheza kama wachezavyo watoto wadogo.
Nyoyo zao zimo katika pumbao, hazizingatii, wameshikilia kuficha njama zao za kumpinga Nabii na Qur'ani, wakiambizana wenyewe kwa wenyewe: Huyu Muhammad si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Na Mtume hawi ila Malaika. Basi, je! Mnamsadiki Muhammad na mnahudhuria baraza za uchawi na hali nyinyi mnaona kuwa hakika huo ni uchawi?
Mtume, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kamjuulisha waliyo kuwa wakiyasema kwa siri, aliwaambia: Mola wangu Mlezi anayajua yote yanayo semwa katika mbingu na katika ardhi, na Yeye ndiye anaye sikia kila linalo sikiwa; na anajua kila linalo tokea..
Bali wao wakasema: Hizi ni mchanganyiko wa ndoto alizo ziota (Muhammad); bali kazua tu na akamsingizia Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Kisha wakaacha hayo na wakasema: Bali huyu ni mtunga mashairi anaziteka nafsi za wenye kumsikiliza. Kama kweli, basi na atuletee muujiza khasa wa kuonyesha ukweli wake, kama walivyo tumwa Manabii wa zamani wakitiwa nguvu kwa miujiza mbali mbali.
Hizo kaumu tulizo ziangamiza baada ya kukadhibisha hiyo miujiza hazikuamini. Basi, je! Watakuja amini hawa yatapo wajia hayo wayatakayo?
Ewe Nabii! Kabla yako wewe hatukuwatumia watu ila watu wa kibinaadamu vile vile, ambao tuliwafunulia Dini waifikishe kwa watu. Basi, enyi mnao kataa! Waulizeni wanazuoni wajuao ilimu za Vitabu vilivyo teremka, ikiwa nyinyi hamyajui hayo.
Wala Sisi hatukuwajaalia Mitume kuwa na miili inayo khitalifiana na miili ya wanaadamu wengine, wakawa wanaishi bila ya chakula, na wakabaki siku zote, na wala hawakuwa wanaishi daima milele.
Kisha tukawatimizia na tukawahakikishia ahadi, na tukawaokoa wao na pamoja nao tukawaokoa tulio taka kuwaokoa miongoni mwa Waumini. Na makafiri walio vuka mipaka tuliwaangamiza kwa kukadhibisha kwao na kuukataa Ujumbe wa Manabii wao.
Sisi hakika tumekuteremshieni Kitabu. Ndani yake yamo mawaidha ya kuwakumbusheni ikiwa mtakisoma na mtayatenda yaliyomo ndani yake. Basi huwaje mkakipuuza na mkakikataa? Je, inda na upumbavu umefika hadi ya kukufikisheni hali hii mlio nayo, mkawa hamuelewi lipi lenye manufaa nanyi mkalikimbilia?