Hakika hawa makafiri wanaipenda dunia, na wanaifadhilisha kuliko Akhera. Na wanaiacha migongoni mwao siku yenye misiba mikubwa, na vitisho vikali. Wala wao hawajui nini cha kuwaokoa wao na hayo!
Sisi tumewaumba wao, na tumefanya kwa hikima kuumbwa kwao. Na tukitaka tutawateketeza wao na tutawaleta mfano ya wao badala yao, ambao hao watakuja kumt'ii Mwenyezi Mungu kinyume na wao.
Hakika Sura hii ni mawaidha kwa walimwengu wote. Basi mwenye kutaka atafuata njia ya Imani na uchamngu kwendea kwa Mola wake Mlezi imfikishe kwenye maghfira yake na Pepo yake.
Wala nyinyi hamwezi kutaka kitu chochote ila wakati anapo taka Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zenu, Mwenye hikima kwa anayo yataka na akayakhiari.
Humuingiza amtakaye katika Pepo yake. Basi kuingia Peponi ni kwa fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu. Naye amewadhalilisha wenye kudhulumu, amewatengenezea adhabu iliyo chungu.